KOCHA GEORGE LWANDAMINA ASEMA ANATAKA KUSUKA YANGA MPYA

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina ametua rasmi tayari kwa kuendelea na majukumu yake, lakini akatamka kwamba sasa amekuja kuisuka timu hiyo huku akisema usajili unaoendelea umemkosha.

Akiongea na saluti5, Lwandamina alisema, katika miezi sita yake ya awali ndani ya Yanga ni kama hakufanya kazi ambapo jukumu zaidi la kuitengeneza Yanga anayoitaka inaanza sasa.  

Lwandamina alisema, kwa sasa analijua soka la Tanzania ambapo anataka kutengeneza Yanga itakayokuwa ngumu kufungika lakini ikawa na wepesi wa kufunga mabao mengi, kazi ambayo haiwezi kumpa shida.

Kocha huyo raia wa Zambia alisema, amekutana na kamati ya usajili ambapo hadi sasa ameridhika karibu na wachezaji wote waliosajiliwa akitaka waendelee na jukumu hilo kukamilisha wachezaji anaowataka waliosalia.

“Nilikuja hapa miezi sita kabla ya Ligi kumalizika. Nimejifunza mengi na sasa nimerudi kuutumikia mkataba wangu. Nataka kusuka Yanga ngumu kwa sasa ambayo itakuwa ni burudani kubwa kwa Wanayanga,” alisema Lwandamina.


“Nimeona usajili unaofanyika, naweza kusema kila kitu kinaenda sawa. Nimeridhika mpaka sasa kupatikana wachezaji niliotaka niwakute, ingawa bado kazi inaendelea.”

No comments