KUTUA KWA AJIBU YANGA NI MUHTASARI TU, HABARI KAMILI INAKUJA

HATIMAYE Yanga imefanya kweli kwa kutangulia kumtambulisha rasmi mshambuliaji wao, Ibrahim Ajibu na hapohapo, mwenyekiti wa kamati ya usajili Yanga, Hussein Nyika akatema cheche akisema bado mashine zaidi inakuja.

Ajibu ametambulishwa rasmi jana makao makuu ya klabu hiyo ambapo nyota huyo aliyetokea Simba, katika tukio lililotanguliwa na kusainishwa mkataba rasmi wa klabu hiyo.

Katika utambulisho huo, mshambuliaji huyo alikabidhiwa jezi yake rasmi atakayoitumia katika maisha yake ya mkataba wa miaka miwili, akikabishiwa na meneja wa kikosi hicho, Afidh Salleh jezi namba 10 iliyokuwa ikivaliwa na mshambuliaji Matteo Anthony ambaye ametolewa kwa mkopo.

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Hussein Nyika amesema ujio wa Ajibu ni kama kufungua milango ya mastaa zaidi kuingia katika kikosi hicho lakini bado kuna majina makubwa yanakuja nyuma yake.

Nyika ambaye kwa sasa ndio gumzo kwa kujua kuwashawishi wachezaji, alisema katika majukumu yao hayo ya usajili akishirikiana na wajumbe wenzake wa kamati hiyo, wanataka kusajili mashine za maana ili ziweze kuendeleza heshima ndani ya klabu yao.


“Tunaendelea na usajili, tumeanza na Ajibu na kazi ndio imeanza hivi. Tunafanya mambo yetu kimyakimya lakini tunapokamilisha tunaweka mambo hadharani. Nataka niwaambie Wanayanga, bado kuna mashine nyingine zinakuja, watulie,” alisema Nyika.

No comments