KYLE WALKER ASEMA GUARDIOLA NDIO MPANGO MZIMA

BEKI mpya wa Manchester City, Kyle Walker amesema kwamba ametua katika timu hiyo kutokana na kuvutiwa na kocha Pep Guardiola.


Walker amesema katika mahojiano baada ya kusaini mkataba mpya kwamba siku zote amekuwa akivutiwa na aina ya ufundishaji wa Pep na kwamba hatua yake ya kutua katika kikosi hicho ni kutimiza ndoto yake ya siku nyingi.

“Kusema ukweli kwa siku nyingi sana nilikuwa natamani kuwa chini ya Pep Guardiola. Huyu ni kocha ambaye nimekuwa nikimtamani sana, anajua kuwanoa wachezaji na kila mchezaji anayepitia kwake anakuwa na kitu cha ziada,” amesema Walker.

Manchester City imezidi kujiimarisha katika safu ya ulinzi baada ya kumwaga dau kubwa la pauni mil 50 kumnasa beki huyo wa kulia ambaye msimu uliopita alikuwa kizingiti kikubwa katika ukuta wa Tottenham.

Beki huyo ambaye anakipiga timu ya taifa ya England pia, amesema kwamba anataka kuwaonyesha mashabiki wa Man City kuwa amefika katika timu ambayo inanolewa na mtu anayemuhusudu.

Tayari Walker alishaichezea Tottenham mechi 228 akiwa White Hart Lane kwa miaka minane mfululizo.

“Kuna jambo ambalo nataka kulionyesha kwa mashabiki wa Man City, lakini nataka pia kumwonyesha kocha kwamba nilikuwa namuhusudu siku nyingi. Siwezi kusema nitayafanya hayo peke yangu lakini najua nitapata ushirikiano kwa watu wengine,” amesema beki huyo.


No comments