LIVERPOOL WAZIDI KUKOMAA NA NABY KEITA WA LEIPZIG

UKISIKIA watu ving’ang’anizi ndio kama Liverpool. Pamoja na kuambiwa kwamba mchezaji Naby Keita hauzwi katika msimu huu, lakini bado wao wanasema kwamba wako tayari kutoa kitita kizito.

Wekundu hao wamekaririwa wakisema kwamba wako tayari kutoa kitita cha kuvunja rekodi kwa ajili ya kumuhamishia kwao nyota huyo kutoka klabu ya RB Leipzig hadi Anfield.

Leipzig wanasisitiza kwamba nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 raia wa Gunea hatauzwa katika kipindi hiki.

Keita anatajwa kwamba thamani yake ya sasa ni pauni mil 70, ingawaje katika mkataba wake kuna kifungu kinachomwachia kwa thamani ya pauni mil 48.

Lakini Liverpool wamesema kwamba Keita ambaye amefunga mabao manane katika msimu uliopita wa Ligi Kuu, lazima atue Anfield.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema kwamba katika kikosi cha sasa na aina ya uchezaji wa kikosi chake, mwanasoka huyo wa Leipzig atakuwa msaada mkubwa.

Kama Klopp atafanikiwa kumwamishia katika kikosi chake katika klabu ya Liverpool, basi wekundu hao watakuwa wamevuka malengo yao ya kusajili kwa kiasi kikubwa.

Majuzi Liverpool wamemsajili kwa pauni mil 34 winga machachari wa Roma, Mohamed Salah ingawa bado usajili wa pauni mil 35 ambao walimsajili Andy Carroll kutoka Newcastle United mwezi Januari mwaka 2011 unasimama kama rekodi.

Wamiliki wa Liverpool, kampuni ya Fenway Sports Group wamemwakikishia Klopp kwamba watampa uwezo mkubwa wa kusajili kikosi matata kwa ajili ya kuimarisha safu yao kuelekea Ligi Kuu msimu ujao na kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

No comments