LIVERPOOL YAPIGA KAMBI YA NGUVU UJERUMANI

KIKOSI cha Liverpool kimekamilika katika maandalizi ya Ligi Kuu England na ile ya mabingwa Ulaya msimu ujao ambapo wekundu hao wameingia nchini Ujerumani kupiga kambi ya nguvu.

Meneja wa kikosi hicho, Jurgen Klopp amesema kwamba sasa kikosi chake ni kama kimekamilika baada ya kurejea kwa washambuliaji Sadio Mane na Danny Ings, lakini pia akiwa na uhakika wa kumtumia kiungo Emre Can.

Mane na Ings wamekuwa wakisumbuka kutokana na majeraha kwa muda mrefu, ingawaje wamekuwa na ushirikiano mkubwa wanapokuwa pamoja dimbani, kisha wakaondoka wote kutokana na majeruhi.

Lakini pia mtu ambaye alikuwa anawaunganisha washambuliaji hao, Can nae alikuwa katika majeruhi na sasa wote wako fiti kwa ziara ya Ujerumani.

Lakini pia beki mpya, Andrew Robertson ambaye amesajiliwa kutoka Hull City kwa uhamisho wa pauni mil 8, nae ameungana na wenzake.

Liverpool imeondoka kwenda Ujerumani ambako itacheza mechi tatu za kirafiki dhidi ya Hertha Berlin, Bayern Munich na ama Atletico Madrid au Napoli ambapo ERobertson ni kama amepata kingeke cha kuanza kutokana na beki chaguo la kwanza, James Milner kusumbuliwa na maumivu.

“Mapema tuliambiwa kwamba tatizo la Milner sio kubwa sana lakini hiyo pia ingetegemea na kocha Jurgen Klopp atakavyomtazama baada ya kupewa ripoti kamili na madaktari,” imesema taarifa fupi ya Liverpool.


Nahodha Jordan Henderson nae amesema kwamba hayuko vizuri sana kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti mara kwa mara ingawaje amesema ni kama amepona kwa asilimia kubwa ndio maana ameanza kucheza.

No comments