LUKAKU ASEMA BADO ANA DENI KWA MOURINHO


ROMELU LUKAKU amesema atafanya kazi kwa bidii zaidi kuliko hapo awali, baada ya kuthibitishwa kwa uhamisho wake kwenda Manchester United ambako atakutana tena na Jose Mourinho.

Mourinho alimpeleka Lukaku  Everton  kwa mkopo mwaka 2014 wakati akiwa kocha wa Chelsea na baadae kumuuza jumla baada ya straika huyo mwenye umri wa miaka 24 kushindwa kung’ara  Stamford Bridge akiishia kucheza mechi 15 bila kupachika bao.

Lukaku alirudi kwenye kilele cha mafanikio baada ya kujiunga na Everton, akifunga mabao 43 katika misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu.

Lakini sasa straika huyo raia wa Ubelgiji anaamini atakuwa ‘levo’ nyingine chini ya Mourinho, ambaye amemtaja kuwa "kocha bora duniani" huku akiweka wazi kuwa bado ana deni la kulipa kwa kocha huyo.

"Sasa ni wakati wa kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa bidii kuliko nilivyofanya kabla. Niko tayari kufanya hivyo na natumaini itakuwa njia nzuri," aliiambia ESPN.


"Najua safari bado ni ndefu, lakini nina nia ya kwenda kwenye njia hiyo na kukamata fursa niliyoipata… Ni klabu kubwa duniani. Ni klabu ambayo ina njaa ya kushinda ligi tena."

No comments