LWANDAMINA ASEMA HAWATAWAFANYIA DHIHAKA SIMBA SC MECHI YA "NGAO YA HISANI" AGOSTI 23

GEORGE Lwandamina ambaye ameipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu uliopita, amesema kuwa hawatarajii kufanya mzaha kwenye mchezo dhidi ya watani wao wa jadi, Simba ambao utachezwa Agosti 23, katika dimba la uwanja wa taifa kabla ya ufunguzi wa michuano ya Ligi.

Kocha huyo amedai kuwa mechi dhidi ya Simba itawapa picha halisi na ndio kipimo watakachotumia kujipima sehemu waliyofikia baada ya kuanza mazoezi makali ya gym jijini Dar es Salaam.

“Kikosi kinaendelea vizuri na mazoezi ya gym ili kujenga stamina ya wachezaji kwa sababu msimu ujao hauko mbali kuanza na tayari tunajua kuna ratiba ngumu ya kushiriki kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika,” alisema kocha huyo.

“Mechi yetu dhidi ya Simba hatuwezi kuibeza kama watu wanavyodhani, tutaingiza kikosi kamili kwa sababu tunataka kuitumia kupima uelekeo wetu, hivyo ushindi wa kila namna ndio mpango wetu namba moja,” aliongeza.


“Najua namna ambavyo hizi mechi huwa zinachukuliwa na mashabiki na zimejaa kila aina ya hisia, hata sisi kama benchi la ufundi tunaheshimu hilo pia na ndio maana tumeanza maandalizi kwa nguvu zote,” alimaliza.

No comments