LWANDAMINA AUNGA MKONO WACHEZAJI WA YANGA KUFANYIWA VIPIMO KABLA YA MSIMU MPYA KUANZA

KOCHA wa kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Geogre Lwandamina ameunga mkono utaratibu unaofanywa na timu yake ya Yanga kuwafanyia vipimo vya kina wachezaji wake kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Kocha huyo alidai kuwa anapenda kufanya kazi na wachezaji wenye stamina kubwa kuweza kuhimili ratiba ngumu ya michuano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Hiki kinachofanyika sasa kwenye kikosi chetu nilikiwaza tangu siku ya kwanza kutua Yanga kwa sababu najali zaidi utimamu wa mwili kwa wachezaji si jambo geni, hata Ulaya wanawafanyia wachezaji vipimo vya kina,” alisema kocha huyo.

“Katika ukanda huu wa Afrika Mashariki nadhani Tanzania kuna ratiba ngumu zaidi ya michuano na kila kocha atahitaji kuwa na kikosi kipana na wachezaji walio fiti kimchezo wakati wote,” aliongeza.

“Msimu uliopita tulibeba ubingwa, tulikuwa na lundo la wachezaji majeruhi nisingependa kuiona hali hii ikijirudia msimu huu,” alimaliza.

Yanga imeanza mazoezi rasmi Jumanne hii katika uwanja wa uhuru maarufu kama "Shamba la Bibi" uliopo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wachezaji waliopitiwa na vipimo vya afya ni pamoja na mshambuliaji Amissi Twambe, Vicent Andrew, Juma Abdul, Said Juma, Yusufu Mhilu na Ibrahim Ajib huku zoezi hilo likidaiwa kuwa endelevu kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo.

No comments