MABONDIA GENNADY GOLOVKIN, CANELO ALVAREZ WAZIDI KURUSHIANA VIJEMBE

PAMBANO la uzito wa kati lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa masumbwi kati ya mabondia Gennady Golovkin dhidi ya Canelo Alvarez, limezidi kushika kasi kutokana na wababe hao kuzidi kurushiana vijembe.

Alvarez, mwenye rekodi ya (49-1-1, 34 Kos), alisema haamini kama anaweza kupoteza pambano hilo, kutokana na maandalizi anayoyafanya hivi sasa. Pambano hilo linatarajiwa kupigwa Septemba 16, 2017, katika ukumbi wa T-Mobile Arena, huko Las Vegas.

Bondia huyo, ambaye siku za karibuni amekuwa akitofautiana sana na chama cha WBC, anatakiwa kupanda ulingoni kuwania mkanda wa WBA pamoja na IBF dhidi ya Golovkin.

"Najivunia kupanda ulingoni kwa ajili ya mchezo huo, ambao nitakuwa nawania mataji muhimu katika mchezo wa ngumi," alisema Alvarez, alipokuwa akifanya mahojiano na wanahabari.

Wakati Alvarez akijitapa, kwa upande wa Golovkin, mwenye rekodi ya (37-0, 33 KOs), ameendelea kujifua kimya kimya, huku promota Tom Loeffler, akisema kuwa naamini Golovkin, atashinda na kubeba taji.

No comments