MADAKTARI AFRIKA KUSINI WATHIBITISHA DONALD NGOMA YUKO FITI KWA ASILIMIA ZOTE

MADAKTARI nchini Afrika Kusini wameridhishwa na afya ya Donald Ngoma hivyo kuwahakikishia Yanga SC kuwa wanaweza kumtumia mshambuliaji huyo.

Ngoma alipewa mapumziko ya miezi minne kuuguza goti ambapo tayari miezi hiyo imeisha huku vipimo vikionyesha amepona kabisa.

Ngoma amerejea nchini akitazamiwa kujiunga na kambi mapema wiki hii.

Ngoma alichelewa kujiunga na timu hiyo baada ya madaktari kumuhitaji kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya mwisho kwenye goti lake.

Mzimbabwe huyo hivi karibuni aliongeza mkataba wa miaka miwili Yanga.

Ngoma alipata majeraha hayo msimu uliopita wa Ligi Kuu na kusababisha ashindwe kuitumikia timu yake kwa asilimia kubwa.

Akizungumza na saluti5, bosi mkubwa wa timu hiyo alisema mshambuliaji huyo ameutaarifu uongozi kuwa atachelewa kutokana na kupitia Afrika Kusini alipokwenda kufanyiwa vipimo hivyo.

Bosi huyo alisema mshambuliaji huyo kikubwa anataka aanze Ligi Kuu akiwa fiti kwa kuhofia kujitonesha.

“Ngoma alichelewa kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake kutokana na kwenda Afrika Kusini katika vipimo vya goti lililokuwa likimsumbua msimu uliopita.”

“Ngoma alianza matibabu hayo ya goti huko Afrika Kusini tangu alipoumia kwa mara ya kwanza baada ya madaktari wa hapa nchini kushindwa kumtibu.”

“Hivyo madaktari hao wamemwitaji tena kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya mwisho kabla ya kumruhusu kuanza kucheza soka,” alisema bosi huyo.

Ngoma alikosa sehemu kubwa ya msimu uliopita kutokana na tatizo hilo la goti.

No comments