MAJERUHI METHOD MWANJALI AREJEA KWENYE UBORA WAKE SIMBA SC

BEKI mahiri wa Simba raia wa Zimbabwe, Method Mwanjali amefuta kabisa matarajio ya baadhi ya mabeki waliokuwa wanawania nafasi yake katika Simba.

Mwanjali ambaye alikuwa atemwe kutokana na kuwa majeruhi kwa muda, mrefu sasa amerejea kwenye ubora wake na kocha wa Simba, Josoph omog amesema kwamba hataki kusikia habari za kutemwa kwa Mwanjali.

Mwanjali ambaye yuko katika kikosi cha Simba kilichoweka kambi nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya, ameonekana mwenye furaha na kiwango chake kimerejea kwa kasi.

Omog amesema kwamba Mwanjali ni mchezaji muhimu na kwamba kama angeachwa kungekuwa na pengo kubwa kwenye safu yake ya ulinzi.

Beki huyo alitoa msaada mkubwa katika safu ya ulinzi ya Simba, hasa mechi za mwanzo wa msimu hadi alipoumia katikati ya msimu.

“Huyu ni mchezaji ambaye anajitambua, anacheza kwa kujiamini na wakati wote huwa msaada kwa timu na kuyafuta makosa ya mabeki wenzake,” alisema Omog na kuongeza:

“Nashukuru kwamba kamati ya usajili iliamua kusikiliza maoni yangu kwamba Mwanjali abaki kwenye kikosi ili kuunganisha wenzake. Nimekuwa nikisema siku zote wakati anakosekana kwenye kikosi kulikuwa na pengo ambalo lilionekana wazi.”

Wakati anaumia kwenye mechi za mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita, Mwanjali aliacha kazi ya ulinzi kwa mabeki wengine Abdi banda, Juuko Murshid na Novat Lufunga, mabeki ambao wote wameondoka Simba. 


Banda amesajiliwa katika timu ya Baroka FC ya Afrika Kusini, Lufunga ameachwa kwenye kikosi hicho na Juuko anakwenda kufanya majaribio nchini Serbia.

No comments