MANCHESTER UNITED WAJIPANGA KUMNG'OA SERGE AURIER PSG

HAKUNA namna! Hivyo ndivyo wanavyosema klabu ya Manchester United ambao wanalazimika kupambana kwa ajili ya kumnasa mtu sahihi wa kucheza kama mlinzi wa upande wa kulia.

Kutokana na ukweli huu, Mashetani Wekundu hao wamepanga kupiga hodi ndani ya klabu ya Paris Saint-Germain na kutaka kumng’oa beki Serge Aurier.

Hatua ya United kumwania Serge inatokana na kugonga mwamba kwa dili la kumsainisha mlinzi hodari wa Monaco, Fabinho.

Serge ameingia katika kurunzi la usajili la kocha Jose Mourinho ambaye anahaha kupata mlinzi wa kulia kabla ya kufungwa kwa dirisha la majira ya kiangazi.

Awali kabla ya Serge, majina mbalimbali yalikuwemo katika orodha ya usajili huo lakini Fabinho ndie aliyekuwa wa kwanza kupendekezwa na Mourinho, lakini dili linadunda kutokana na klabu ya Monaco kutaka kitita cha maana kwa ajili ya beki wao huyo.

Monaco walihitaji kitita cha pauni mil 40 kwa ajili ya timu inayomwitaji Fabinho anayewaniwa pia na Atletico Madrid.
Kocha wa United, Jose Mourinho amekiri kukwama kwa dili la Fabinho na sasa anahamishia nguvu zake kwa Serge mwenye umri wa miaka 24 sasa.

Raia huyo wa Ivory Coast amekuwa katika kiwango ambacho Mourinho anaamini ndie mtu sahihi wa kuimarisha kikosi cha msimu huu.


Hata hivyo, Manchester United wameweka mezani ofa ya pauni mil 25 kwa “Mmatumbi” huyu, ingawa klabu yake ya PSG inataka dau la pauni mil 35 kwa ajili ya kupata saini yake.

No comments