MAZOEZI MAKALI YA LWANDAMINA YAMZIMISHA KINDA WA KIKOSI B YANGA

MASHABIKI wa Yanga wamekoshwa na mazoezi makali ya kocha George Lwandamina lakini wakati mwenyewe akisema kazi bado haijaanza, kinda mmoja akajikuta akipoteza fahamu katika mazoezi hayo.

Kilichotokea ni kwamba katika mazoezi hayo yalifanyika juzi na kuwa makali kwa muda wa masaa matatu, Lwandamina alionekana kutaka kuwajaza upepo wachezaji wake kwa kukimbia katika vituo tofauti.

Wakati mazoezi hayo yakiendelea kinda mmoja wa kikosi B alijikuta akishindwa kumaliza na kuanguka kabla ya kupatiwa huduma ya kwanza ya haraka.

Kinda huyo alilazimika kitibiwa kisha kuondolewa katika mazoezi hayo hali ambayo iliwafurahisha mashabiki wengi wakiamini kocha wao huyo amedhamiria kuisuka timu imara.

Akizungumzia mazoezi hayo, Lwandamina amesema bado kikosi chake hakijaanza mazoezi magumu ambapo kazi kubwa itakuwa katika kambi yao Morogoro.


“Watu wasione yale ni mazoezi magumu, tulichokuwa tunafanya ni kupanua mapafu na uwezo wa moyo kufanya mapigo yakae sawa lakini kazi kubwa bado, tutakuwa na wakati mgumu tutakapokuwa kambini nataka kutengeneza timu na kawaida timu yangu inapomaliza mazoezi kama haya kuwa haifungiki,” alisema Lwandamina.

No comments