MOURINHO: NATAKA MAKUBWA ZAIDI KUTOKA KWA MARTIAL

KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba anataka makubwa zaidi kutoka kwa staa wake, Anthony Martial, licha ya kung’ara katika mchezo wa kuamkia juzi ambao Manchester United waliibuka na ushindi dhidi ya Real Madrid.

Katika mchezo huo uliopigwa katika mji wa San Clara uliopo katika Jiji la California, Martial alionesha kiwango cha hali ya juu kilichoiwezesha Man United kuondoka na ushindi huo wa mabao 2-1 kwa mikwaju ya penalti, baada ya miamba hiyo kutoshana nguvu kwa kupata sare ya bao 1-1 dakika za kawaida za mtanange huo wa michuano ya mabingwa wa kimataifa ambayo ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya msimu ujao.

Msimu uliopita straika huyo wa timu ya Taifa ya Ufaransa alishindwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Man Utd, baada ya kuwasili msimu wa 2015-16, lakini usiku huo wa kuamkia jana akaonesha kiwango cha hali ya juu kilichowafanya mabingwa hao wa Ligi ya Europa kupata bao la kuongoza kabla ya kipindi cha pili.

Martial aliambaa na mpira na kisha kuwalamba chenga mabeki watatu wa Real Madrid kabla ya kumtengenezea pande Jesse Lingard, ambaye aliukwamisha kirahisi na kimiani lakini akakosa mkwaju wa penalti.

"Ni dhahiri tunataka uwiano zaidi katika kipaji chake, nadhani leo (juzi) ilikuwa chanya kwake, ndiyo sababu nimemwacha kwa muda wa dakika 90 uwanjani, alifurahia na kujaribu vitu," alisema Mourinho.

"Ni muhimu kujaribu vitu katika mchezo wa kirafiki kama huu hivyo ilikuwa ni vizuri kwa Anthony na kujiamini kwake. Yeye bado ni kijana mdogo, bado ana muda wa kujifunza, kujiiramisha na vilevile kujijenga,” aliongeza Mreno huyo.


Alisema anachoweza kueleza ni kwamba, staa huyo amefanya mazoezi vizuri zaidi tofauti na mwanzo na amejituma na sasa kilichobaki ni kuonesha kipaji chake zaidi katika njia inayotakiwa.

No comments