MUUMIN ATIA CHUMVI KWENYE KIDONDA TWANGA PEPETA …amwambia Asha Baraka asiwabane wasanii kupiga ndondo Jumanne


Mmiliki na mwimbaji wa bendi ya Double M Plus, Mwinjuma Muumin amemtaka mmiliki wa Twanga Pepeta, Asha Baraka awaachie wasanii wake wafanye show za ‘ndondo’ siku za Jumanne.

Muumin amesema ameshangazwa sana kitendo cha Asha Baraka kuwa mkali kwa wasanii wake kufanya kazi nje ya bendi siku za Jumanne.

Hivi karibuni wasanii karibu wote wa Twanga Pepeta walianza mpango mpya wa kupiga show za kila Jumanne kwa kushirikiana na bendi ya taarab ya Wakali Wao inayomilikiwa na Thabit Abdul, lakini Asha Baraka akasema wazi kuwa jambo hilo halikubali na kama litaendelea basi hatua stahiki zitachukuliwa kwa wasanii hao.

Katika maongezi yake na Saluti5, Muumin akasema: “Nikiwa kama msanii na mmiliki wa bendi, naomba mkurugenzi mwenzangu Asha Baraka apunguze kuwabania wasanii wake, hali ya maisha ni ngumu asiwafanyie roho mbaya wafanyakazi wake.

“Nimesoma Asha Baraka akisema show zenyewe ni za kuingiza 20,000 tu, hazitamsaidia chochote msanii. Hivi kweli Asha Baraka anaidharau elfu ishirini usawa huu? Hajui kama kwa mwezi hiyo itakuwa ni elfu themanini? Je elfu themanini haitoshi kulipa kodi ya nyumba?

“Mkurugenzi wangu wa zamani anatakiwa abadilike sasa, asiwabane sana wasanii maana akiendelea hivyo asishangae Mapacha Watatu nyingine ikizaliwa.

“Nakumbuka hata Mapacha ilizaliwa rasmi baada ya Asha Baraka kuwabania wasanii wake wasifanye show za Jumanne ambazo Twanga huwa inapumzika. Asha Baraka asilazimishe historia ijirudie.”.

No comments