MWAKYEMBE AWATAKA TAIFA STARS KUELEKEZA NGUVU MECHI DHIDI YA RWANDA

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewataka wachezaji timu ya soka ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kuelekeza nguvu katika mchezo dhidi ya Rwanda ili waitoe na kusonga mbele kwenye michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika “Chan”, baada ya mafanikio ya Kombe la Cosafa.

Taifa Stars imewasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana alfajiri ikitokea Afrika Kusini ambako walishiriki mashindano ya Kombe la Cosafa na kumaliza katika nafasi ya tatu.

Na katika mapokezi ya timu hiyo, waziri Mwakyembe alikuwepo majira ya saa 9 za usiku sambamba na kaimu rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na akawapongeza kocha Salum Mayanga na wasaidizi wake pamoja na wachezaji kwa mafanikio hayo.

“Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa kutupa heshima katika nchi yetu kwa hatua mliyofikia, nina furaha sana na karibuni tena nyumbani na ninawaomba muelekeze nguvu zenu katika mashindano yajayo ili kuiletea nchi yetu maendeleo katika soka,” alisema Mwakyembe.


Kwa upande wake, kocha Mayanga amesema kwamba wanamshukuru Mungu kwa mafanikio hayo na sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo dhidi ya Rwanda kuwania tiketi ya kucheza fainali za ubingwa wa Mataifa ya Afrika “Chan”.

No comments