MWANAHAWA CHIPOLOPOLO AKAMILISHA "NILIJUA YATAKUSHINDA" NDANI YA HALICHACHI CLASSIC

STAA wa mipasho mwenye sauti ya kumtoa nyoka pangoni, Mwanahawa Chipolopolo amefunguka na kusema kuwa amemaliza kazi ya kufanyia mazoezi kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Nilijua yatakushinda’.

“Hii itakuwa kazi yangu ya kwanza ndani ya bendi yangu mpya ya Halichachi Classic Modern Taarab, nawaomba mashabiki waupokee kwa mikono miwili ujio wangu huu mpya,” amesema.

Chipolopolo amesema kuwa, kibao hicho ambacho muziki wake umetengenezwa na Amour Maguru, kitaanza kutambulishwa rasmi wiki hii kwenye kumbi mbalimbali watakazotumbuiza.

Amesema kuwa, kibao hicho kinaweza kuwa cha kihitoria kwa mwaka huu kutokana na namna kinavyopangiliwa kwa ustadi mkubwa kwenye sauti na ala.

Ndani ya ‘Nilijua Yatakushinda’, Chipolopolo anawapasha ‘mapaparazi’ wote kuwa, mapenzi yao sio ya kuchovya na kuwataka wacheze mbali na chokochoko zao zenye nia ya kuwatenganisha.


“Kibao hicho tunatarajia kukirekodi mwishoni mwa mwezi huu baada ya kutambulishwa kwenye kumbi nyingi zaidi na mashabiki kukitolea maoni mbalimbali,” amesema Chipolopolo.

No comments