Habari

MWANAMUZIKI JIMMY MANZAKA ADAI KAANGUSHIWA KIPIGO NA CHRISTIAN BELLA …Bella asema hizo ni kiki za kijinga

on

Mwimbaji wa kujitegemea wa miondoko ya rumba Jimmy Manzaka amedai
kuangushiwa kipigo na wafuasi wa Christian Bella kwa kile anachoamini kuwa ni
wivu kutokana na ujio wake wa nyimbo mbili kali.
Manzaka raia wa Congo ambaye amekuwa akifanya shughuli za muziki huko
Dubai, yupo Tanzania kwa miezi kadhaa akipika albam yake ya rumba ambapo tayari
ameachia nyimbo mbili “Shilawadu” na “Coco Channel”.
Mwimbaji huyo mwenye undugu na Nyoshi el Saadat anadai kipigo hicho
kilitokea takriban siku kumi zilizopita Sinza jijini Dar es Salaam nyumbani kwa
Christian Bella.
Manzaka anadai alikwenda kumtembelea Nyoshi ambaye anaishi jirani na
Christian Bella ambaye amedai pia kuwa wanafahamiana vizuri.
Jimmy Manzaka anasema baadae alikaa kwenye pub moja ya jirani akipata
kinywaji na rafiki zake na ndipo alipomuona Bella akirejea nyumbani kwake hivyo
akaamua kwenda kumsalimia kwa kuwa ni rafiki yake.
“Bella alikuwa anarejea safari kutoka nje ya Dar, nikaenda kumsalimia,
tukaongea vizuri kisha nikarejea pub kuendelea kunywa na rafiki zangu, lakini
muda mfupi baadae akaja mtu na kuniambia kuwa Bella ananiita nyumbani kwake,”
anaeleza Jimmy Manzaka katika mazungumzo yake na Saluti5.
“Baada ya kufika nyumbani kwake Bella akaanza kunishutumu kuwa mimi
namsema vibaya kwa watu, namtangazia kuwa alikosa watu kwenye show zake za
Bukavu, Congo.
“Nikajaribu kujitetea lakini haikusaidia, watu wake wakanikaba na
kuanza kunipiga huku Bella akisema yeye ndiyo mwenye Dar es Salaam, yeye ndiyo
rais na anaweza kunifanya lolote kwa kuwa mimi ni mshamba na siwezi kushinda na
yeye,” alifunguka Jimmy Manzaka ambaye pia alionyesha picha zake zenye makovu
sehemu za shingoni kuthibitisha kile alichofanyiwa nyumbani kwa Bella.
Hata hivyo Bella alipoulizwa na Saluti5 juu ya tuhuma hizo, alisema
hizo ni kiki za kijinga.
Bella anasema hajawahi kumwalika nyumbani kwake Jimmy Manzaka kwa kuwa
hawana ukaribu huo na wala sio rafiki yake.
“Kama anasema alipigwa nyumbani kwangu basi aeleze vizuri alikwenda
kufanya nini. Sijawahi kumwalika kwangu, kama alijipeleka mwenyewe na kukutana
na wasaidizi wangu wasiomfahamu, hiyo mimi sina namna ya kumsaidia,”anaeleza
Bella.
“Wasaidizi wangu waliniambia kuna mtu mlevi aliingia ndani kwa nguvu
na kulazimisha kuonana na mimi, wakambwambia Bella hayupo lakini bado akawa
mbishi kutoka, wakamtoa nje kwa nguvu, sijapewa taarifa kuwa mtu huyo
alipigwa,” anafafanua Bella na kuhoji ni vipi mtu aingie kwa nguvu nyumbani kwa
mtu kama njia za kutafuta kiki.
“Kama kweli alipigwa basi aseme amechukua hatua gani, alikwenda
kuripoti kituo kipi cha polisi, alitibiwa hospitali gani. Kwangu mimi hizo
naziona ni kiki za kizamani sana, atafute njia nyingine ya kutokea,” anaeleza
Christian Bella kupitia maongezi ya simu na Saluti5.

Comments

comments

About Saluti 5

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *