MWANAMUZIKI MKONGWE ROY MUKUNA AFARIKI DUNIA


Mwanamuziki mkongwe, bingwa wa kupuliza saxophone, Roy Mukuna (pichani juu) amefariki dunia leo asubuhi katika hospitali ya taifa ya Muhimbiliji jijini Dar es Salaam.

Roy Mukuna aliyetamba zaidi na bendi ya Maquis du Zaire (Maquis Original), alilazwa Muhimbili kwa siku kadhaa kufuatia kusumbuliwa na tatizo la ini.

Kabla ya kupelekwa Muhimbili, Roy Mukuna alikuwa akiugulia nyumbani kwake Mburahati Barafu.

Hadi kifo chake, Mukuna alikuwa rais wa bendi ya Super Kamanyola ya Mwanza ambayo ameitumikia kwa miaka mingi kabla ya kuzidiwa na kurejeshwa Dar es Salaam wakati wa mapumziko ya mwezi wa mtukufu wa Ramadhan mwaka huu.

Aidha, kabla hajarejeshwa Dar es Salaam, mwanamuziki huyo alikuwa akitibiwa Mwanza ambapo kwa takriban miezi sita, hakuweza kuonekana kwenye jukwaa la Super Kamanyola.
Mukuna aliyezaliwa Zaire (Congo) mwaka 1947, alizitumikia bendi za Super Matimila na Tanza Muzika.

Msiba uko nyumbani kwake Mburahati Barafu jijini Dar es Salaam lakini mtoto wa marehemu, Emmy ameiambia Saluti5 kuwa bado hawajakaa kama familia na kupanga siku ya mazishi.

“Tutazika Dar es Salaam, lakini siku ya mazishi tutawajuza baadae, bado hatujakaa kama familia na kupanga taratibu za mazishi,” alisema Emmy.

No comments