NEYMAR ASEMA MSIMU UJAO NI MUHIMU SANA KATIKA MAISHA YAKE


“MSIMU ujao ni muhimu sana katika maisha yangu.” Hivyo ndivyo alivyosema supastaa wa Barcelona na Brazil, Neymar katika mahojiano na mtandao wa ESPN Brasil.

Katika msimu ujao, straika huyo wa miaka 25, atamkaribisha kocha mpya Camp Nou baada ya msimu ulisiopendeza chini ya Luis Enrique.

Msimu ujao pia utakuwa na fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia, ambako Brazil itakuwa na kazi ya kufuta aibu ya kichapo cha mabao 7-1 ilichopata nyumbani ilipokutana na Ujerumani hatua ya nusu fainali.

Neymar, ambaye alisaini mkataba mpya mnono wa miaka mitano na Barcelona Oktoba mwaka jana, anasema atakuwa tayari.

"Natumaini utakuwa msimu na mafanikio mengi na furaha nyingi," alisema na kuongeza kuwa ataanza kujiandaa kuukabili.

No comments