OMOG ASEMA HANA KISINGIZIO CHA SIMBA KUBORONGA LIGI ITAKAPOANZA

KOCHA wa Simba, Joseph Omog amesema kwamba kwa namna anavyoiona timu hiyo, hatakuwa na kisingizio tena cha timu yake kufanya vibaya wakati Ligi Kuu itakapoanza.

Kocha huyo ameitazama Simba inavyofanya mazoezi nchini Afrika Kusini ikiwa kwenye utulivu wa hali ya juu na kusema kwamba kama kuna watu wanadhani kuwa timu hiyo iko vibaya wanatakiwa kutafakari upya.

Lakini amesema atajisikia amani zaidi baada ya kuitazama timu yake ikicheza mechi mbili za kirafiki katika ardhi hiyo ya Nelson Mandela na ndipo atajua aanzie wapi.

Omog anawasubiri wachezaji kadhaa ambao usajili wao bado haujakamilika lakini ikidaiwa kwamba wakati wowote kuanzia sasa wachezaji wawili wataungana na wenzao.

Wanaotarajiwa kujiunga na wenzao hao ni pamoja na Nicholas Gyan, mshambuliaji mpya raia wa Ghana ambaye habari zinasema kwamba ameshafanyiwa mipango ya usafiri wa moja kwa moja kutoka Ghana hadi Afrika Kusini.

Gyan ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ghana, Asamoah Gyan, anacheza katika timu ya Ebusua Dwarfs FC na ni mmoja wa wachezaji wanaoongoza kwa ufungaji mabao katika Ligi Kuu ya Ghana.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 19 anatajwa kwamba ameshamalizana na Simba na amepewa mkataba wa miaka miwili kuwatumikia wekundu hao wa Msimbazi.

Mchezaji mwingine anayesubiriwa kwa hamu ni Haruna Niyonzima ambaye ameachana na klabu yake ya zamani ya Yanga na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na Simba wakati wowote.


Omog amesema, wachezaji hao pamoja na Emmanuel Okwi ambaye tayari ameshasaini ndio ambao wanasubiriwa.

No comments