PICHA 8 ZA WASANII WA TWANGA PEPETA WALIVYOJILIPUA JANA SIKU NA KUKAIDI AMRI YA BOSI WAO


Zaidi ya asilimia 80 ya wasanii wa Twanga Pepeta jana usiku walishiriki onyesho la pamoja na bendi ya taarab ya Wakali Wao ndani ya ukumbi wa Friends Corner Bar, Manzese jijini Dar es Salaam.

Wasanii hao walishiriki onyesho hilo kinyume na amri ya bosi wao Asha Baraka ambaye hapo awali aliimbia Saluti5 kuwa haungi mkono wasanii hao kushiriki show hiyo.

Asha Baraka akaenda mbali zaidi kwa kusema hata onyesho la Jumanne iliyopita baina ya bendi hiyo mbili, lilifanyika bila idhini yake.

Kuelekea onyesho la jana, Asha Baraka akasema Twanga Pepeta haitashiriki onyesho hilo ambalo hapo awali lilitangazwa kuwa litakuwa likifanyika kila Jumanne ndani ya ukumbi huo wa Friends Corner huku likipewa jina la “Usiku wa Wababe”.

Hata hivyo wasanii hao wa Twanga Pepeta walikuwa waungwana ambapo walitii amri ya bosi wao ya kutopeleka bendi (African Stars – Twanga Pepeta) na badala yake wakaenda kushiriki wao wenyewe bila jina la bendi wala vyombo vya bendi – karoso nyimbo tu.

Naam nyimbo za Twanga Pepeta ndizo zilizosikika Friends Corner jana usiku ambapo mwimbaji na rapa  Khalid Chokoraa akasikika akitupia rap inayosema: “hii ndondo, hii ndondo”.

Mwimbaji Kalala Jr naye akachombeza: “Wazee wa Kujilipua, wazee wa kujitoa muhanga, kila Jumanne tuko hapa hata usiposikia tangazo, usiku kibabe Ndondo Jazz Band na Wakali Wao”.

Kwa upande wake Ally Chocky yeye akasema: “Tukiwa kule ni Twanga Pepeta lakini tukiwa hapa sisi ni Wakali Wao Jazz Band kwahiyo kila Jumanne utakuwa unapata show ya Wakali Wao Modern Taradance na Wakali Wao Jazz Band”.

Mmoja wa wasanii walioshiriki onyesho hilo akaiambia Saluti5 kuwa hawakukaidi amri ya bosi wao maana wao wamekwenda kama wasanii wa Twanga Pepeta na hawakwenda kama bendi ya African Stars “Twanga Pepeta”.

“Tunamheshimu sana bosi wetu na kamwe hatuwezi kukiuka amri yake hasa ukizingatia kuwa Jumanne bendi yetu huwa haifanyi kazi,” alisema msanii huyo.


Hadi kamera ya Saluti5 inaondoka ukumbini hapo, sura za wasanii wakubwa wa Twanga Pepeta ambazo hazikuonekana jukwaani ni Luizer Mbutu, Hajj BSS na God Kanuti, lakini mastaa wengine wote walikuwepo.

Waliokuwepo ni pamoja na Ally Chocky, Kalala Jr, Chokoraa, Jojoo Jumanne, James Kibosho, Miraji Shakashia, Victor Nkambi, Super Nyamwela, Maria Soloma, Mapande na Chiku Kasika bila kusahau jeshi la kukodiwa J Four Sukari.
 Ally Chocky katika ndondo ya jana usiku
 Khalid Chokoraa akiwajibika jukwaani
 James Kibosho akicharaza drums na fulana yake ya Twanga Pepeta
 Jojoo Jumanne kwenye bass
 Kalala Jr akiwachezesha madansa wa Twanga
 Kutoka kushoto ni Super Nyamwela, Chiku Kasika, Mapande na Maria Soloma
 Miraji Shakashia na gitaa la solo
 Victor Nkambi wa Twanga akipapasa kinanda jana usiku
Ally Chocky, Chokoraa, Kalala Jr na J Four Sukari

No comments