RAHEEM STERLING ATABIRI MAKUBWA MENGI MAZITO MAN CITY KWA USAJILI WA GUARDIOLA

MSHAMBULIAJI wa pembeni wa klabu ya Manchester City, Raheem Sterling amemtabiria makubwa kocha wake, Pep Guardiola katika usajili anaoufanya wakati huu wa majira ya joto.

Sterling ameweka wazi kuwa kikosi hicho kwa sasa kimekamilika kuelekea msimu mpya wa Ligi, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao ambao unatarajiwa kuanza Agosti.

Mara ya mwisho klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England ilikuwa 2014 lakini msimu uliopita ilimaliza ikishika nafasi ya tatu ikiwa nyuma ya pointi 15 dhidi ya mabingwa wa Ligi hiyo, Chelsea.

Hadi sasa tayari Manchester City imeonyesha jeuri ya fedha kwa kuzinasa saini za wachezaji watatu, mlinda mlango Ederson Moraes kutoka Benfica kwa kitita cha pauni mil 34.7, kiungo kutoka Monaco, Bernardo Silva kwa pauni mil 43 na beki kutoka Tottenham, Kyle Walker kwa uhamisho wa pauni mil 50.

Sterling anaamini kwa usajili wa wachezaji hao, Guardiola atafanikisha kufanya makubwa msimu ujao japokuwa bado kocha huyo anaendelea kutafuta baadhi ya saini za wachezaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na mshambuliaji wa Arsenal, Alexis Sanchez.

“Kilichobaki kwa sasa ni kutwaa mataji msimu ujao, tunataka taji la Ligi Kuu, hicho ni kitu muhimu sana kwangu mwakani kwa kuwa tuna kikosi bora nchini England.”


“Guardiola amefanya makubwa katika usajili wakati huu wa majira ya joto na ninaamini bado yuko kwenye mipango ya kuendelea kukiongezea nguvu ili kuweza kufanya makubwa zaidi, sina wasiwasi na msimu ujao, ninaamini tuna nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa,” alisema Sterling.

No comments