RAIS WA KLABU BRAZIL AJIUZURU KUTOKA NA VITISHO VYA MASHABIKI

RAIS wa klabu ya Paysandu Sport ya nchini Brazil amelazimika kuachia ngazi kutokana na vitisho vya mashabiki wa timu hiyo, taarifa ya BBC inasema.

Rais huyo, Sergio Serra katika taarifa yake ya kujiuzulu amesema kwamba watu waliojiamini wametishia kumuua iwapo klabu yake hiyo itashuka daraja.

Sergio Serra amesema kuwa alifuatwa akitembea na familia yake na watu waliokuwa katika pikipiki na kutishiwa kwamba ole wake timu ishuke daraja.

Paysandu ina makao yake huko Belem na ni miongoni mwa klabu kubwa Kaskazini mwa Brazil.

Klabu hiyo imekumbwa na wakati mgumu na iko katika nafasi ya 16 katika Ligi ya Serie B, ikiwa nafasi moja pekee kushushwa daraja.

Christina Serra, dada yake Sergio aliripoti katika mitandao ya kijamii kwamba nduguye alikuwa ameenda kujivinjari na mkewe pamoja na watoto siku ya Jumapili.

Mmoja wao ambaye alikuwa ameziba uso wake na shati akamwambia kuwa: “Najua unakoishi, iwapo Paysandu itashuka daraja hadi serie C nitakuua wewe na mkeo na mwanao.”

“Ndugu yangu alishituka na kuamua kufanya maamuzi ya kujiuzulu.”

Soka ya Brazil imekuwa na wakati mgumu kukabiliana na ghasia ya mashabiki kwa miongo kadhaa na wachezaji pia wamekuwa wakipokea vitisho.


Mwaka 2011, aliyekuwa beki wa kushoto, Robert Carlos alisema kuwa amepokea vitisho vya simu na watu wamekuwa wakilifuata gari lake wakiwa katika pikipiki baada ya klabu yake ya soka ya Corinthians kubanduliwa katika Kombe la Copa Libertadoris.

No comments