RAPHAEL VARANE AONYESHA DALILI ZOTE ZA KUMFUATA MOURINHO OLD TRAFFORD

TAARIFA za tetesi za usajili za mwishoni mwa juma zinamtaja nyota wa Real Madrid, Raphael Varane kuwa na asilimia kubwa ya kutua katika kikosi cha mashetani wekundu wa Old Trafford.

Ukubwa wa tetesi hizi unafuatia ukweli mwingine pia kuwa Varane ana mawasiliano na kocha wa United, Jose Mourinho.

Imefahamika kuwa Mourinho amemweka katika orodha ya usajili wake pindi akichukua jukumu la kukinoa kikosi cha United.

Kwa mujibu wa Daily Star, imemwelezea Varane kama ni mchezaji wa awali aliye katika malengo ya Mourinho na kwamba wawili hao wameshaanza kuteta.

Hata hivyo, United wanakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa vigogo wengine wa soka barani Ulaya ambao nao wameweka nia ya kumsainisha beki huyo.

Mabingwa wa Bundesliga, Bayern Munich, Liverpool, Juventus na Paris Saint-Germain wamo katika mbio za kuwania saini ya Raphael Varane.

Varane amekuwa akikosa namba ya kudumu katika kikosi cha Los Blancos cha msimu huu baada ya kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane kuwapa nafasi kubwa walinzi Sergio Ramos na Pepe.

Varane mwenye umri wa miaka 23, ameelezwa kutoficha mapenzi aliyonayo kwa kocha Jose Mourinho tangu akiinoa Chelsea.

Hata alivyokuwa ndani ya Real Madrid, Mourinho alikuwa akimwamini Varane kiasi cha kupangwa mara kwa mara, tofauti na sasa ambapo amekuwa akipangwa kwa nadra na Zidane.

No comments