"RASTA" ANAYESAKWA NA YANGA ASEMA DILI LAKE LA KUTUA JANGWANI LIKO UKINGONI

KIUNGO mpya anayetafutwa na Yanga, Kabamba Tshishimbi amefunguka kwa mara ya kwanza kwamba dili lake la kuja kujiunga na timu hiyo lipo katika hatua za mwisho na kwamba mara atakapotua anataka kufanya kweli katika klabu hiyo bingwa nchini.

Kabamba ambaye ni raia wa DRC Congo anayekipiga katika klabu ya Mbambane Swallows ya Swaziland, alisema tayari mazungumzo yake na viongozi wa Yanga yapo katika hatua ya mwisho na kilichobaki ni kumalizana tu.

Kabamba ambaye anajulikana kwa jina "rasta" alisema endapo dili hilo litakamilika kwake hajakosea kukubali kuja kutumikia timu hiyo ambapo amefuatilia taarifa zake na kuona sio timu inayokosa mafanikio kutokana na kushiriki mara kwa mara mechi za mashindano ya Afrika.

Kiungo huyo alisema kwa sasa mkataba wake na Swallows umebakiza miezi miwili na kwamba hana mpango wa kubakia katika timu hiyo akisubiri kumalizana na Yanga ili aweze kuja kuitumikia.

“Nimefanya mawasiliano na hao Yanga sio kwa mara moja, tunaongea sana nafikiri naweza kuja huko kama tukimalizana, hiyo ni timu kubwa naiheshimu sana kutokana na rekodi yake nimeona kila mara inashiriki mashindano ya Afrika,” alisema kabamba.

“Hapa mkataba wangu unamalizika baada ya miezi miwili, wanataka nibaki lakini nimewaambia nina mipango yangu kwahiyo nataka nione kwanza namalizana vipi na Yanga ili niwaambie rasmi kwamba sasa naondoka nataka kuja kuitumikia Yanga.


No comments