RONALDO AWEKA WAZI TAARIFA ZA KUPATA WATOTO MAPACHA... asema sasa ruksa kuitwa "baba wawili"

BAADA ya tetesi kusambaa kuwa staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo amepata watoto mapacha hatimaye straika huyo ameamua kuweka wazi kuwa taarifa hizo ni za kweli na kwa sasa anaweza kuitwa baba wawili.

Ronald aliweka wazi taarifa hizo juzi wakati akiwakilisha timu yake ya taifa katika mashindano ya mabara yanayoendelea kutimua vumbi nchini Russia.

Hata hivyo akiweka wazi taarifa hizo ambazo ni njema kwake lakini alikuwa akisononeka baada ya Ureno kujikuta ikipokea kipigo cha mabao 3-0 kwanjia ya penati baada ya kushindwa kufungana na Chile katika muda wa kawaida wa mchezo huo wa nusu fainali.

“Nilikuwa katika majukumu ya timu ya taifa kama ilivyo mara zote nikitumikia mwili wangu na uwezo wangu wakati watoto wangu wawili walipozaliwa,” aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa facebook.

“Kwa bahati mbaya hatukuweza kutimiza malengo yetu makuu ambayo tulikuwa tunayataka, lakini nina hakika tutaendelea kuwapa raha Wareno,” aliongeza kupitia ujumbe huo.

“Rais wa Shirikisho la soka la Ureno na timu yote ya taifa watakuwa na mawazo kuwa imeniumiza na kwamba siku hii sitaisahau,” aliongeza tena staa huyo.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kusononeshwa na kutolewa nje katika michuano hiyo, lakini anafurahi kwani kwa mara ya kwanza atakwenda kuwaona watoto wake.


Mtoto wa kwanza wa Ronaldo aitwaye Cristiano Ronaldo Jr. alitimiza miaka saba mapema mwezi huu.

No comments