RUVU SHOOTING YATANGAZA KUIKAZIA SIMBA MECHI YAO YA UFUNGUZI WA LIGI KUU MSIMU HUU

BAADA ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania bara kutangazwa, Uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting umetamba kupata ushindi ili kuwavurugia mipango wapinzani wao Simba ya kuanza vizuri.

Ruvu Shooting watafungua pazia na Simba katika mchezo wao unaotarajiwa kupigwa Agosti 26, mwaka huu uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa klabu hiyo, Masau Bwire alisema watahakikisha wanapambana ili kupata pointi tatu muhimu na kuwatoa Simba katika mpangilio wao wa kuanza na ushindi katika mechi ya awali.

“Nimeiona ratiba ya Ligi Kuu na ipo vizuri, lakini mipango yetu ni kuanza kwa ushindi, hivyo Simba wasitarajie kupata ushindi kirahisi katika mchezo huo kwani tumepanga kuwavuruga katika mechi ya kwanza,” alisema.

Alisema kikosi hicho kimeingia kambi muda mrefu kujiandaa na msimu mpya huku wakiwa bado wanaendelea na mchakato wa usajili kwa wacheazji wapya.


Bwire aliendelea kusema hadi sasa bado hawajasajili wachezaji wowote kwani wanataka kufanya taratibu na kupata wachezaji watakaosaidia timu hiyo kwenye msimu mpya.

No comments