SCOTT PARKER ATUNDIKA DARUGA AKIWA NA MIAKA 36

KIUNGO wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya England, Scott Parker ameamua kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 36.

Parker alianzia kibarua chake kwenye klabu ya Charlton Athlatic na mechi yake ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1997 kabla ya Januari 2004 kujiunga na klabu hiyo ya Stanford Bridge.

Hata hivyo alishindwa kupata namba kwenye kikosi cha kwanza alipokuwa na Chelsea na Julai 2005 akaamua kuondoka na kujiunga na Newcastle United na kisha akaweza kuonyesha uwezo wake akiwa na timu za Westham United, Tottenham na Fulham.

“Uamuzi wa kustaafu sio moja ya jambo rahisi kwa upande wangu, lakini kwa muda mrefu nimelijadili nikiwa na marafiki zangu na ninaamini kuwa sasa ni muda mwafaka kufungua ukurasa mwingine katika maisha na kazi zangu,” aliandika Parker kupitia taarifa aliyoitoa hivi karibuni.


“Wakati naanza kukipiga nikiwa na timu ya Charlton Athletic kwa muda wa miaka yote nilikuwa na ndoto za kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili, nafikiri ni jambo la kheri nimeweza kufurahia kazi yangu. Najivunia kwa hilo na kusema ukweli nimekuwa na furaha kipindi chote hicho,” aliongeza kiungo huyo.

No comments