SIMBA SC YAJINADI KUWA KAMILI GADO KWA AJILI YA LIGI KUU

BAADA ya kupata wachezaji wawili wa kigeni, Simba imejinadi kuwa sasa ipo kamili na imetimia tayari kwa michuano ya Ligi Kuu bara na ile ya kimataifa.

Simba imesisitiza kuwa imemaliza kazi baada ya kupata majembe mawili ya maana na sasa inaanza rasmi maandalizi ya uwanjani huku nyota wengi wapya wakiahaidi kufanya kazi ya uhakika.

Kikosi kizima cha Simba kimeondoka Jumanne hii kuelekea Afrika Kusini watakakoweka kambi ya wiki tatu kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.

Simba ambayo imefanya usajili wa wachezaji tisa mpaka sasa, imebakiza usajili wa wachezaji wawili tu ili hesabu ya usajili ifungwe kwa upande wao.

Habari kutoka Simba zinasema kuwa timu hiyo imeondoka na wachezaji wake wote ambao hawapo kwenye majukumu ya timun ya taifa ambapo mjumbe mmmoja wa kamati ya utendaji klabuni hapo alisema kambi hiyo imefadhiliwa na wanachama wa klabu hiyo na mfadhili wao, Mohammed Dewji “MO”.

Ikiwa Afrika Kusini Simba itacheza mechi tatu za kirafiki na timu za huko na itarejea nchini Agosti 5, kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya Simba Day itakayo fanyika Agosti 8.

Wachezaji ambao mpaka sasa Simba imewasajili ni magolikipa wawili Aishi Manula na Emmanuel Mseja, mabeki Shomary Kapombe, Ally Shomary, Jamali Mwambeleko, Salim Mbonde na Yussuf  Mlipili huku washambuliaji wakiwa ni John Boko na Emmanuel Okwi.

Wachezaji wa Simba ambao wapo kwenye majukumu ya timu ya taifa ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Salim Mbonde, Mzamiru Yassin, Said Mdemla, Shiza Kichuya na John Bocco ambao wataungana na wenzao kwenye kambi Julai 24, baada ya mechi dhidi ya Rwanda wikiendi hii.


Hata hivyo mjumbe huyo wa kamati ya utendaji amesema Simba itafunga daftari lake kwa kufanya usajili wa shindo ambao utatikisa Afrika Mashariki na Kati.

No comments