SIMBA YASHUSHA STRAIKA MWINGINE KUTOKA GHANA

KLABU ya soka ya Simba ni kama imenogewa na wanandinga wa kutoka nchini Ghana ambapo sasa imeshusha straika mwingine na taarifa zilizopo ni kwamba amepelekwa kambini nchini afrika kusini.

Wachezaji wa wekundu hao kwa sasa wapo nchini Afrika Kusini kwa kambi ya siku 20 ya kujiandaa na Ligi Kuu sambamba na ile tamasha la kila mwaka la Simba Day linalofanyika kila ifikapo Agosti 8.

Taarifa za ndani zinazohusiana na masuala ya usajili zinasema kuwa raia huyo wa Ghana ni Thomas Agyei ambaye ni mpachika mabao ambaye Simba iliripotiwa kumtuma mjumbe mmoja kwenda kumalizana nae huko kwao.

Agyei ambaye pia ni mchezaji kijana ameripotiwa kukamilisha hatua muhimu za kujiunga na kikosi cha Mnyama msimu huu ambapo mara baada ya kutaarifiwa ujio wake amekuwa akisubiliwa kwa hamu.

Habari ambazo bado ni motomoto zinasema kuwa kocha Joseph Omog ameridhishwa na kiwango chake kupitia CD ya aina ya uchezaji wake na ameuagiza uongozi ufanye hima kumpandisha pipa ili kuwahi kambi ya Sauzi.

Omog amehitaji uharaka wa kupelekwa kwa straika huyo kama njia ya kwenda kujiridhisha na kiwango katika kambi hiyo ya kujiandaa hatua ambayo uongozi umeitikia wito wa kocha wao huyo.

No comments