SINGIDA UNITED KUJIPIMA NA MECHI 10 KABLA YA MICHUANO YA LIGI KUU

KLABU ya Singida United iliyopanda daraja msimu uliopita imenunua basi la mil 300 ili kurahisisha safari zake pindi michuano ya Ligi Kuu bara itakapoanza kutimua vumbi.

Singida United imepanga kucheza mechi kumi za kujipima nguvu kabla ya msimu kuanza ambapo katika michezo hiyo, wanatarajia kucheza dhidi ya timu tano za Tanzania bara na tano za kimataifa.

Mkurugenzi wa klabu hiyo, Festo Richard alithibitisha taarifa hizo na kusema kuwa wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya timu kutoka nje ya mipaka ili kucheza mechi za kujipima kabla ya Ligi kuanza.

“Tumepanga kuwashangaza watu, ndio maana mambo yetu yanakwenda kama yalivyopangwa. Tutacheza mechi tano za kirafiki dhidi ya timu za nje kisha tutacheza nyingine tano za ndani,” alisema mkurugenzi huyo.

“Tutaingia kambini jijini Mwanza kabla ya kuanza kwa michezo hiyo, lakini kwa hivi sasa bado hatujajua ni timu zipi tutacheza nazo hapa nchini kwani bado tunaendelea kufanya nazo mazungumzo, ila timu za nje zitatoka kwenye mataifa jirani na Tanzania,” aliongeza.

“Tunataka kupeleka mambo yetu kisasa, ukiachiliambali wafadhili tuliokuwa nao hivi sasa tunatarajia kupata wengine saba ambao bado mazungumzo yanaendelea mpaka wakati huu,” alimaliza.


Timu ya Singida United imepanda daraja msimu huu na inaonekana kuanza kufanya maandalizi ya nguvu huku ikifanya matumizi makubwa ya fedha katika usajili wake ambapo imekuwa ikinasa mastaa kutoka nje ya nchi.

No comments