SKASSY KASAMBULA AENDELEA KUMLILIA SHAABAN DEDE

KIFO cha aliyekuwa mwimbaji mwandamizi wa Msondo Ngoma Music Band, Shaaban Dede kimeonekana kumshitua mwimbaji mwenzie nguli, Skassy Kasambula ambaye kwa sasa anafanya shughuli zake za muziki nchini Kenya.

Katika video iliyotumwa mwishoni mwa wiki kwenye grupu la Whatssaap la Friends of SIKINDE, Skassy anaonekana kutoa kwa majonzi mazito salamu za pole kwa wanamuziki walioko Tanzania, huku akisema kuwa msiba huu ni wa Afrika Mashariki nzima.

“Kwa kweli nachukua fursa hii kutoa salamu zangu za pole kutokana na msiba mkubwa uiliotukumba sisi wanamuziki kwa kumpoteza ndugu yangu, rafiki yangu Super Motisha “Tingisha” shaaban Dede,” amesema Skassy.

“Tulifanya nae kazi pale Safari Sound (OSS) “Ndekule” wakati ule katika wimbo wake “Nyumba ya Mgumba”.”

“Kabla hatujarekodi huu wimbo, aliyekuwa anaimbisha huu wimbo ni yeye na Fresh Jumbe, Jumbe alipoondoka uongozi wa bendi na yeye Dede wakaamua kunitwisha jukumu la kipande cha Jumbe nikiimbishe mimi Studuio na tulivyomaliza kurekodi walinipongeza na kunambia kazi nzuri nimefanya.”


“Kwa kweli ni masikitiko makubwa sana ndugu zangu. Huu ni msiba mkubwa sana umetukumba sisi Watanzania. Nipo hapa Kenya sasa ni miaka 20, toka 1997 kikazi tu lakini makazi bado ni Tanzania. Poleni sana ndugu zangu watanzania na wanamuziki wenzangu, poleni sana,” alimaliza Skassy.   

No comments