THEO HERNANDEZ 'AUMBULIWA' NA DANADANA AKITAMBULISHWA RASMI REAL MADRID


THEO HERNANDEZ, 19, amejikuta akipunguza utamu wa sherehe yake ya kutambulishwa akiwa ingizo jipya Real Madrid katika usajili wa kiangazi hiki, baada ya kushindwa kuhalalisha thamani yake ya pauni milioni 20 kwa kutaabika kupiga danadana ndani ya Santiago Bernabeu mwanzoni mwa wiki.

Mfaransa huyo anayecheza beki ya kushoto, alisema kuwa alikuwa 'na furaha sana kuwa kwenye klabu bora duniani', lakini licha ya shauku yake hiyo, hakuwa na uwezo wa kukonga nyoyo za mashabiki waliojazana Bernabeu baada ya kumudu kupiga danadana sita pekee.

Hernandez aliyetokea Alaves alikocheza kwa mkopo msimu uliopita, alipiga danadana nne vizuri kabla kupiga ‘fyongo’ ya tano na mpira ukapaa juu alipopiga ya sita, hivyo kuamua kuudaka na kugeukia umati wa mashabiki kuwapungia huku akionekana kufedheheka.

No comments