TOTO TUNDU AANZA MAKEKE KIBAHA CARNIVAL BAND... aachia mduara mkali wa "Kaumia"

MWIMBAJI nguli wa muziki wa dansi ambaye mwishoni mwa mwaka jana aliamua kuhamishia mabegi ndani ya bendi ya Kibaha Carnival, Mhina Panduka “Toto Tundu” ameanza kufungua makucha.

Kiongozi wa jukwaa wa Kibaha Carnival, Iddy Moro aliyeongea na Saluti5 jijini Dar es Salaam, amesema kuwa tayari Toto ameshaiipulia bendi hiyo kibao kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Kaumia’.

“Kibao hicho kipo katika miondoko ya mduara na tayari tumeanza kukirindimisha kwenye kumbi mbalimba,li za burudani tunapofanya shoo,” amesema Iddy ambaye ni kati ya waimbaji hatari kwa sasa.

Iddy amesema kuwa, wataingia studio kurekodi kibao hicho muda si mrefu, baada ya mipango ya kamati kuu ya bendi hiyo kukaa sawa, ambapo amewaomba mashabiki kukaa mkao wa kusubiri ujio mpya wa Toto Tundu.


Kabla ya kutua ndani ya Kibaha Carnival inayokusanya pia wakali kama Chacha Tumba, Joniko Mafuta na Awadh Key body, Toto Tundu alikuwa na JKT Ruvu sambamba na baadhi ya wasanii waliojiengua kutoka Twanga Pepeta.

No comments