VIWANGO VYA WACHEZAJI SINGIDA UNITED VYAMKUNA HANS PLUIJM

KOCHA wa timu ya Singida United, Hans Van der Pluijm ameelezea kuridhishwa na viwango vya wachezaji wake baada ya kucheza mechi mbili za kujipima nguvu za kushinda zote.

Kikosi cha Singida United kimeweka kambi ya mwezi mmoja jijini Mwanza na tayari kimecheza mechi za kirafiki dhidi ya Pamba FC na Alliance Academy, huku wachezaji wakionyesha kandanda la hali ya juu.

Katika mchezo wa kwanza Singida iliibamiza Pamba 5-0 kabla ya mwisho wa wiki kuifumua Alliance mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Elisha Muroiwa dakika ya 10 na Tafazwa Kutinyu dakika ya 74.

Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema licha ya kikosi cha Alliance kuwa bora, wachezaji wake walicheza soka safi linalompa matumaini ya kufanya vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania bara utakaoanza Agosti 26, mwaka huu.

“Tulicheza vizuri ingawa mechi ilikuwa ngumu sana, Alliance ni timu nzuri yanye wachezaji wengi wenye vipaji, nimeridhika na matokeo tuliyopata,” alisema Pluijm.

Aidha Pluijm aliongeza kuwa wanatarajia kukutana ili kupanga ratiba ya kucheza mechi ya kirafiki katika nchi ya Uganda au Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo DRC.

Alisema mikakati yao kwa sasa ni kuhakikisha wanapambana kwa hali na mali ili kujiwekea mazingira ya kumaliza Ligi ya msimu ujao wakiwa nafasi za juu kwenye msimamo.


Agosti 6 mwaka huu Singida wanatarajia kuvaana na mabingwa wa Ligi Kuu, Yanga katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments