WABABE WA TWANGA PEPETA WASALIMU AMRI KWA ASHA BARAKA …wabwaga manyanga show za Jumanne


Kwa Jumanne mbili mfululizo, zaidi ya asilimia 80 ya wasanii wa Twanga Pepeta walikuwa wakishiriki onyesho la pamoja na bendi ya taarab ya Wakali Wao ndani ya ukumbi wa Friends Corner Bar, Manzese jijini Dar es Salaam.

Taarifa za ndani zikadai kuwa wasanii hao walishiriki maonyesho hayo kinyume na amri ya bosi wao Asha Baraka ambaye hapo awali aliimbia Saluti5 kuwa haungi mkono wasanii hao kushiriki show hizo.

Asha Baraka akaenda mbali zaidi kwa kusema kuwa hata onyesho la Jumanne ya kwanza (Julai 11) baina ya bendi hizo mbili, lilifanyika bila idhini yake.

Kuelekea onyesho la pili (Julai 18), Asha Baraka akasema Twanga Pepeta haitashiriki onyesho hilo ambalo hapo awali lilitangazwa kuwa litakuwa likifanyika kila Jumanne ndani ya ukumbi huo wa Friends Corner huku likipewa jina la “Usiku wa Wababe”.

Hata hivyo wasanii hao wa Twanga Pepeta wakawa wajanja ambapo waliamua kutopeleka bendi (African Stars – Twanga Pepeta) na badala yake wakaenda kushiriki wao wenyewe bila jina la bendi wala vyombo vya bendi – kasoro nyimbo tu, hatua ambayo pia ilishutumiwa vikali na Asha Baraka.

Waliokuwepo kwenye show hiyo ni pamoja na Ally Chocky, Kalala Jr, Chokoraa, Jojoo Jumanne, James Kibosho, Miraji Shakashia, Victor Nkambi, Super Nyamwela, Maria Soloma, Mapande na Chiku Kasika bila kusahau jeshi la kukodiwa J Four Sukari.

Kuelekea onyesho la tatu (Julai 25), mkwara mkali ukapitishwa kuwa msanii wa Twanga Pepeta atakayeshiriki onyesho hilo basi ajihesabu kuwa amejiengua kundini. Mkwara ukasaidia na hakuna msanii wa Twanga Pepeta aliyetia timu Friends Corner ukiondoa wasanii wachache wanaoitumikia bendi hiyo kama madeiwaka.

Na sasa kuelekea onyesho la nne (August 1), tangazo la show limewaondoa wasanii wa Twanga Pepeta na badala yake Wakali Wao Modern Taarab watasindikizwa na mfalme wa kibao kata, Kivurande Junior sambamba mkali wa singeli MC Soud.

 Tangazo la onyesho la August 1 linavyosomeka

No comments