WENGER ADAI PSG WAMEMSHINDWA ALEXIS SANCHEZ

KOCHA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, amefunguka na kusema matajiri wa klabu ya PSG, wameshindwa kuinasa saini ya mshambuliaji wake, Alexis Sanchez na wamegeukia kwa staa wa Barcelona, Neymar.

Kocha huyo amesisitiza kwamba, anapambana kuhakikisha Sanchez anaendelea kuwa ndani ya kikosi chake katika kipindi hiki cha uhamisho wa wachezaji japokuwa klabu mbalimbali bado zinaendelea kuwania saini yake.

Kulikuwa na taarifa kwamba, Sanchez wiki hii anatarajia kukutana na viongozi wa PSG ili kuzungumza juu ya uhamisho wake, lakini Wenger ameweka wazi hakuna mipango yoyote ambayo itafanyika.

“Sina uhakika kama Sanchez atakuwa mjini Paris au alikuwa huko. Najua kwamba PSG hawawezi kuipata saini ya Sanchez na ndio maana wanapambana kuipata ya mshambuliaji wa Barcelona, Neymar.

“Nimekuwa nikisoma habari mbalimbali kutoka kwenye magazeti ya nchini Ufaransa kama vile L'Equipe, siku tatu au nne zilizopita zote zilikuwa zinawazungumzia Sanchez na Neymar. Leo hii wameacha kumzungumzia Sanchez na wanamzungumzia Neymar.

“Akili yangu kwa sasa ipo sawa, kila kitu nilikieleza wazi kwamba mchezaji huyo hawezi kuondoka kwa sasa ndani ya kikosi chetu, kwa upande wangu ninaamini hivyo,” alisema Wenger.

Hata hivyo, kupitia akaunti ya Instagram ya beki wa klabu ya Barcelona, Gerard Pique, aliposti picha akiwa na Neymar na kuandika kwamba ‘haendi kokote, atabaki Nou Camp.’

PSG wameonesha nia ya kuitaka saini ya Neymar kwa kiasi cha Euro milioni 222 ikiwa ni ada ya uhamisho, huku pauni 596,000 ni sehemu ya mshahara wake kwa wiki ambao ni zaidi ya bilioni 1 na milioni 720 za Kitanzania.

Hata hivyo, baadhi ya wachezaji wa Barcelona, Lionel Messi, Luis Suarez na wengine wanajaribu kufanya mazungumzo ya kumshawishi mchezaji huyo aendelee kuwa kwenye kikosi hicho kwa msimu ujao.

Mashabiki wengi wa Barcelona wanatumia mitandao ya kijamii na ‘kushare’ picha yake huku ikiwa na ujumbe wa kumtaka mchezaji huyo abaki kikosini, ila wapo ambao wanataka mchezaji huyo aondoke ili kiasi hicho cha fedha kitumike kuongeza wachezaji wengine katika kipindi hiki cha usajili.

No comments