YANGA SASA YASAKA SAINI ZA MASTAA WANNE KABLA DIRISHA LA USAJILI KUFUNGWA

KAMATI ya usajili ya klabu ya Yanga imepitisha majina ya mastaa wengine wanne inaowasaka kwa udi na uvumba kabla ya kufungwa kwa dirisha hili kubwa la usajili wa wachezaji.

Klabu hiyo ambayo imeanza mazoezi ikijiandaa na michuano ya Ligi Kuu Bara na Klabu Bingwa Afrika inaendelea kufanyia kazi ripoti ya kocha wao, George Lwandamina ambapo inaonyesha bado kuna mastaa wengine wane ambao wanatakiwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho chenye jukumu la kutetea ubingwa msimu ujao.

“Tunafanya kazi kwa umakini wa hali ya juu kwa kushirikiana na benchi la ufundi, mashabiki wanapaswa kutulia na hasa katika kipindi hiki ambacho tunasaka nyota wengine ili kukamilisha matakwa ya kocha,” alisema mwenyekiti wa kamati ya usajili, Hussein Nyika.

“Yapo maeneo manne ambayo kocha aliyaainisha na sisi kama kamati tunayafanyia kazi kabla dirisha halijafungwa, ili kupata kikosi bora msimu ujao, tunayo majina tayari na tutaweka wazi baada ya kuwanasa, kwasababu hivi sasa kuna hatua zinaendelea kufanyika,” aliongeza.


Ripoti zilizopo ni kuwa klabu hiyo inataka kusajili nyota wawili kutoka kwenye Ligi ya Afrika Kusini pamoja na wengine wawili kutoka Tanzania, lakini mpaka hivi sasa majina hayajawekwa wazi moja kwa moja.

No comments