YANGA YAIPANIA SIMBA SC NGAO YA HISANI AGOSTI MWAKA HUU

KUFUATIA zoezi la usajili linaloendelea kufanywa kimyakimya na uongozi wa klabu ya Yanga ambayo imeachana rasmi na beki Vincent Bossou raia wa Togo, Katibu mkuu Charles Mkwasa amesema kuwa hilo haliwafanyi kusahau umuhimu wa mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya watani wao, Simba.

Miamba hiyo miwili inatarajia kukutana kwenye mchezo huo Agosti 19, mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza baada ya misimu mitatu kupita.

“Ndio. Hatufanyi usajili kwa mbwembwe kama wenzetu, tunaendesha mambo kisayansi huku tukiweka akili katika mchezo wetu dhidi yao Agosti 19,” alisema Mkwasa ambaye amewahi kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars.

“Ni mchezo muhimu sana kwetu kwa sababu unaweza kurejesha hali ya kikosi kabla ya kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu na Klabu Bingwa Afrika, nadhani mechi na Simba ni kipimo kizuri kwa timu za hapa nchini,” aliongeza.


Yanga ambayo imebeba ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya tatu mfululizo itakutana na Simba iliyobeba Kombe la FA kwa mara ya kwanza, huku zote pia zikiwa na tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu huu.

No comments