YANGA YAWAPOZA MASHABIKI WAKE KUHUSU PENGO LA MSUVA

YANGA inafahamu kwamba itampoteza straika wake Simon Msuva, lakini uongozi umewatoa wasiwasi mashabiki wake kwa kuwaambia kwamba yuko mtu mwenye uwezo zaidi yake ambaye anakuja Jangwani.

Klabu hiyo ya Jangwani imetangaza kuinasa saini ya winga mmoja matata sana mwenye mbio na uwezo mkubwa wa kupiga krosi kwa ajili ya kuwatengenezea mapande mastraika hatari akina Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Ibrahim Ajib.

Winga teleza huyo mpya aliyenaswa na mabosi hao wa Yanga ni Issa Yahya Akilimali ambaye walimdaka juu kwa juu na kuamua kumficha moja kwa moja katika maeneo tulivyo ya jiji la Dar es Salaam ili kumpa mkataba wa kuitumikia timu hiyo.

Sifa za winga huyo mpya ni kwamba ana uwezo mkubwa wa kumiliki mipira, kukimbia kwa kasi, kupiga krosi zenye macho sambamba na kufumua mashuti kulenga lango kama alivyo Msuva aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita akilingana na Abdullahman Mussa wa Ruvu Shooting ambapo kila mmoja alitupia kambani mara 14.

Yanga awali walianza kumuona kwenye michuano ya Ndondo Cup akiwa na timu ya Kigoma All Stars lakini walipotaka kumsainisha wakasikia kwamba anatakiwa na Lipuli ya Iringa.

Hata hivyo kwavile viongozi wa Yanga walikuwa tayari wameshamuona uwezo wake wakaamua kumng’ang’ania na kulazimika kusitisha kila kitu ilimradi kuinasa saini yake, jambo ambalo wamekwishalifanikisha.

Dogo huyo alikuwa akisoma nchini Uganda na alipomaliza ndipo alipoamua kurejea nchini na kuanza kufanya mavitu yake.


Kutokana na umuhimu wa usajili wa kiberenge huyo, kocha George Lwandamina aliamua kumjaribisha na kumuona anafaa kumrithi Msuva anayeenda Morocco kucheza soka kulipwa.

No comments