ABDI BANDA AANZA KUNAWIRISHA KIBARUA CHAKE AFRIKA KUSINI

BEKI aliyefanya kazi kubwa akiwa Simba kwa misimu kadhaa, Abdi Hassan Banda ameanza kuitumikia klabu yake mpya ya Bakora FC inayocheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwa mafanikio.

Juzi beki huyo ameinusuru timu yake hiyo kulala kwenye uwanja wake wa nyumbani mbele ya Orlando Pirates ya kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Uganda, Miluti Sredojevic "Micho" baada ya kuifungia bao la kusawazisha katika sare ya 1-1.

Bakora FC waliokuwa  nyumbani walikubali kuruhusu bao katika dakika ya 41 baada ya Thabo Qalinge kuifungia Orlando bao la kwanza.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini ulifanyika uwanja wa Peter Mokaba jijini Johannesburg, Abdi Banda aliyejiunga na timu hiyo mwezi Juni akitokea Simba ya Tanzania alifunga bao hilo dakika ya 73 kwa kichwa kufuatia mpira wa kona ya juu.

Kama  kawaida yake, Banda alikwenda kusaidia mashambulizi baada ya kuona mafowadi wanakosa mabao ya wazi na kweli akafanikiwa kufunga bao hilo ambalo lilishangiliwa kwa nguvu na mashabiki waliojazana kwenye uwanja huo.


Tovuti ya klabu hiyo imemsifu Banda kutokana na aina yake ya uchezaji wa kutumia akili nyingi uwanjani kiasi kwamba tangu ajiunge na klabu hiyo kuna mafanikio yanayoonekana.

No comments