AJIB AWEKA WAZI MAWINDO YAKE KWA SIMBA NGAO YA JAMII


BAADA ya kuonyesha kiwango cha juu katika michezo ya hivi karibuni akiwa na timu yake mpya ya Yanga, mshambuliaji Ibrahim Ajib sasa anaiwinda Simba kuelekea kwenye mchezo wao wa kesho wa Ngao ya Jamii.

Ajib alicheza kwa kiwango cha kuvutia kwenye michezo ya kirafiki ambayo Yanga imeshacheza hadi sasa.

Mara baada ya michezo hiyo, Ajib aliweka wazi kuwa akili yake kwa sasa inafikiria mchezo wa Ngao ya Jamii ambapo Yanga itakutana na mahasimu wao kwenye soka la Tanzania, Simba.

“Kwa sasa naiwinda Simba, ili nionyeshe ubora wangu, hivyo siwezi kuzungumza sana, cha msingi mashabiki wetu waje kwa wingi Agosti 23 ili waje kushuhudia uhondo wakati tukimuadhibu mnyama,” alinukuliwa Ajib.

Mashabiki wa Yanga ambao walijitokeza kwenye michezo hiyo ya kirafiki, walisifia uwezo wa Ajib na kusema kwamba, wana uhakika msimu huu ataisaidia sana Yanga. 

“Nimemuona Ajib akiichezea Yanga kwa mara ya kwanza dhidi ya Singida United, nimelizika na kiwango chake na hivyo sina shaka kabisa kwamba Agosti 23 Simba lazima tuwaadabishe na yeye namuamini atafanya kweli kwa timu yake hiyo ya zamani,” alisema shabiki wa Yanga aliyejulikana kwa jina Mohamed Juma.

No comments