AYA 15 ZA SAID MDOE: BENDI ZA ‘TWISHENI’ NI UKOMBOZI AU KABURI LA MUZIKI DANSI NA TAARAB?


Wenyewe wanajifananisha na walimu waliojiriwa katika shule  fulani  fulani lakini wakajitafutia fursa ya kuendesha masomo  ya ziada (tuition/twisheni) ili kujiongezea kipato.

Lakini pia wanajifananisha na madaktari walioajiriwa katika mahospitali makubwa huku wakifanya kazi za ziada kwenye zahanati zao binafsi. Wanajifananisha pia na wanasoka wakubwa wanaoshiriki michuano ya mchangani – Ndondo.

Na pengine kuna siku pia watajifananisha  na wapiga debe wa vituo vya mabasi ambao  hawachagui wala hawana basi maalum la kulipigia debe.

Ninaowazungumzia hapo ni wanamuziki wa dansi na hata wale wa taarab ambao wamekithiri kwa tabia za 'ukinyonga', hawajulikani wana rangi gani, hawafahamiki wako bendi gani.

Leo  utamuona bendi hii, kesho bendi ile, keshokutwa bendi nyingine ...msanii mmoja ndani ya wiki moja anaonekana katika bendi tatu na mbaya zaidi tungo anazozunguuka nazo  kote huko ni zilezile. Hakuna ubunifu mpya.

Ukimuuliza anakwambia mimi ni msanii wa bendi fulani, lakini kule kwingine  naongeza maslahi tu, ni kamradi kangu ka pembeni, sawa na twisheni tu.

Nawaza iwapo mfumo huu una msaada wowote kwa muziki wa dansi na taarab, najaribu kujiuliza iwapo aina hii ya ufanyaji kazi ni ukombozi au ni kaburi kwa bendi zetu ambazo kila kukicha zimekuwa zikikabiliana na hali ngumu inayosabishwa na ukame wa mashabiki kwenye kumbi zao.


Niliwahi kusema kuwa tatizo kubwa la wasanii wetu wengi ni shule ndogo na ni kama vile hawakutegemea kuwa hapo walipo, haikuwa ndoto waliyoisaka kwa udi na uvumba na ndio maana hawana muda wa kuyalinda mafanikio yao… wanaishia kuwa malimbukeni na mazumbukuku tu.

Wasanii wa dansi na taarab wana kazi kubwa ya ‘kuji-brand’ na kwa kuendelea kwao kuamini kuwa umaarufu unalindwa kwa kuwa kiguu na njia kwenye kila kumbi ya starehe, kuganga njaa kwenye kila show, basi ni wazi kuwa miaka michache ijayo tutashuhudia utitiri wa bendi za twisheni huku maonyesho halisi ya bendi yakiota mbawa na hapo ndipo tutakapojua kama mfumo huu ni ukombozi au ni kaburi.

Ifike wakati sasa wanamuziki wetu wawekeze akili zao katika kuwa na kazi mbadala, kuwa na njia nyingine ya kuongeza kipato nje muziki.

Kupiga misele huku na huko na kudandia show za ndondo si suluhisho la kujikwamua na hali ngumu ya uchumi bali kujipeleka wenyewe kwenye chumba cha wangonjwa mahututi (ICU).

Ifike wakati wanamuziki wetu wajiulize ni kipi walichosahau kwenye bendi fulani hadi wakarudisha mpira kwa kipa, halafu watueleze kwanini baada ya kurudisha mpira kwa kipa wanatafuta tena njia ya kuondoka.

Kama wangekuwa wanajiuliza vizuri kabla ya kuchukua hatua, ni wazi tusingekuwa tunashuhudia bendi hizi za twisheni, kama wangekuwa wana washauri wazuri tusingeshuhudia utitiri wa show za ndondo ambazo hazina kichwa wala miguu.

Hakuna ubishi kuwa ni kweli wamiliki wengi wa bendi wamekuwa wazito kutekeleza makubaliano juu ya maslahi ya msanii, hakuna ubishi kuwa ni kweli wasanii wengi wanaishi kwa mfumo wa kibarua kwenye bendi zao, lakini hili haliwezi kurekebishika kwa kuibuka kwa bendi za twisheni na show za ndondo, bali linaweza kumalizwa kwa wasanii kuingia mikataba ya kisheria na waajiri wao, mikataba itayolinda maslahi ya pande zote mbili.

Msanii anaishi kwenye bendi kwa mwaka mzima, hajatunga hata mstari mmoja wa wimbo, hana uhakika wa kuongeza hata mashabiki 20 kwenye bendi yake, lakini yeye ndiyo anakuwa wa kwanza kulalamika kuwa tajiri yake anawanyonya na hapo ndio unapoona umuhimu wa kuwepo mikataba itakayoonyesha msanii ataifanyia nini bendi na bendi itamfanyia nini msanii.

No comments