AYA 15 ZA SAID MDOE: KWANINI CHRISTIAN BELLA? KWANINI LAKINI?


SHOW ya Jumamosi usiku pande za BL Park, Tabata Kinyerezi kutoka kwa Malaika Band chini ya Christian Bella, iliashiria jambo kubwa – muziki wa dansi bado unakubalika, tatizo ni kukubalika kwa bendi au msanii sambamba na maandalizi ya kisomi.

Mfalme huyo wa masauti na bendi yake wakapiga show iliyoshuhudiwa na umati mkubwa wa watu kwa kiingilio kikubwa cha shilingi 10,000 na 20,000, kwa jicho la haraka haraka kulikuwa na zaidi ya watu 1200 ukumbini.

BL Park ni kiota ambacho kimekuwa kikitumika kwa show za bure kutoka bendi kubwa za Tanzania lakini siku hiyo ya Jumamosi waandaaji wakawa na uthubutu wa kuandaa show ya kiingilio cha pesa, wakaingia gharama kubwa ya maandalizi na mwisho wa siku juhudi zao zikazaa matunda.

Mafanikio ya show ya Bella ni kama ‘matusi’ kwa bendi zingine za dansi ambazo zinapumulia gesi kwenye maonyesho yao, hamasa ya mashabiki wa Bella ikathibitisha namna wapenzi wa muziki wanavyotaka tungo nzuri.

Ilikuwa ni kama vile Bella hakuhitaji waitikiaji kwenye bendi yake kwani kazi hiyo ilifanywa na mashabiki ambao waliimba kwa nguvu viitikio vya nyimbo zote za Bella na kufanya isisimue sana.

Pesa alizomiminiwa Bella jukwaani zinaweza kabisa kukodi hata show za bendi mbili za dansi kwani kwa hesabu za haraka haraka, jamaa aliondoka na zaidi ya shilingi milioni mbili jukwaani.


Unaweza ukaona kama nafanya udaku kusema pesa aliyotuzwa jukwaani inaweza kukodi show mbili za dansi, lakini nani asiyejua kuwa bendi nyingi kubwa sasa hivi zinalipwa kati ya shilingi laki tano hadi saba ili kwenda kupiga show za kiingilio kinywaji?

Namna maegesho ya magari ya BL Park yalivyochafuka kwa utitiri wa vyombo hivyo vya moto, unadhifu wa mashabiki na ‘fujo’ za vinywaji na vyakula kwenye meza zao, wingi wa mastaa wenye majina yao kwenye onyesho hilo, kulidhihirisha kuwa Christian Bella ana utajiri wa mashabiki wenye ‘nyadhifa’.

Kupitia onyesho lile, kipo cha kujifunza kwa mameneja wa bendi na mapromota, ipo haja ya kujiuliza iwapo kudumaza akili zetu kwenye show za kiingilio kinywaji ni kuukwamua muziki wa dansi au kuudidimiza.

Majuzi kuna kampuni moja ya pombe ilialika bendi tatu kubwa za dansi kwenye bar fulani maeneo ya Sinza kwa kiingilio kinywaji (bure), lakini mahudhurio yaliyopatikana yalikuwa ya kawaida sana.

Nimekuwa nikiwaza siku zote kwanini nyimbo za bendi zetu hazichezeki? Kwanini muziki wa dansi ugeuke kuwa muziki wa kuusikiliza mithili ya taarab asilia? Kwanini bendi zetu hazijiulizi ni njia gani ametumia Bella kuuruka mtego huo? Kwanini Christian Bella? Kwanini lakini?

Mashabiki wanajazana kwenye dancing floor kucheza nyimbo za Bella, mashabiki ukumbini wanawehuka na huyu jamaa na kuimba nyimbo zake kwa hisia kali utadhani walizitunga wao.

Nilichogundua ni kwamba ubunifu duni na kukosa uvumbuzi wa fikra mpya  kwa wanamuziki, mameneja na mapromota ni miongoni mwa mambo mengi makubwa yanayofanya muziki wa dansi uendelee kuduma na kugeuzwa kuwa chombo cha kuuzia pombe.

Ukitaka kuamini kuwa bendi zetu zimelala na hazina fitna, hebu jiulize ni wapi uliona mrejesho wa show ile ya bendi tatu za dansi pale Sinza? Wapi uliona matokeo ya show? Kwenye gazeti? TV? Blogs? Kilichothaminiwa pale ilikuwa ni kuuza pombe tu. Hivyo ndivyo muziki wa dansi unavyolinganishwa na taulo la hotel.

Iko haja ya bendi zetu kujipanga upya ikiwa kweli zinataka kukabiliana kidhati na mabadiliko na ushindani uliko sasa, vinginevyo Christian Bella ataendelea kuwaburuza, ataendelea kubaki kwenye sayari ya peke yake ndani ya soko la muziki wa dansi.

No comments