AYA 15 ZA SAID MDOE: MUZIKI WA DANSI UMEBAKIA KUWA ZILIPENDWA?


Wakati nchi nzima ikitekwa na moja ya nyimbo mpya za bongo fleva zilizoachiwa hivi karibuni, “Zilipendwa” inayokumbushia vitu vingi vilivyovuma huko nyuma kabla havijapitwa na wakati, nami nachukua fursa hiyo kuuliza muziki wa dansi nao zilipendwa?

Asubuhi ya Alhamisi fulani hivi karibuni kupitia kipindi cha “Joto la Asubuhi” cha kituo cha radio cha EFM nilibahatika kusikiliza wimbo wa “Elimu ya Mjinga” wa TOT Plus utunzi wake marehemu Banza Stone, nikafurahi sana namna watangazaji walivyokuwa na mzuka wa hali ya juu na wimbo huo.
        
Mtangazaji Mussa Kipanya, kijana ambaye ni mjuzi nisiyekuwa na shaka naye kwenye muziki wa dansi, akaongoza hamasa zilizotia mshawasha wakati wimbo huo uko hewani, akaonyesha namna anavyofahamu kila kipande cha wimbo huo.

Lakini baada ya wimbo huo kumalizika nikamsikia akiwasimulia watangazaji wenzake kwa unyonge: “Gerald (Hando) huu muziki wa dansi jamani, yaani ukiangalia historia ya muziki wa dansi, dah wee wacha tu…” Mtangazaji mwenzake Adela Tilya ambaye naye bado ni binti mbichi, akachombeza: “Siku hizi hakuna tena haya mambo”.

Kwa tafsiri nyepesi tu ni kwamba kauli hizo mbili kutoka kwa watangazaji hao ambao bado si wahenga, inaonyesha wazi kuwa muziki wa dansi umebakia kuwa historia. Bila shaka walimaanisha kuwa muziki wa dansi ulikuwepo zamani sio sasa hivi ambapo tungo za kuliteka soko la muziki zimeota mbawa.

Hii ndio hatari ya muziki huu, wahenga wanautaka na kuufagilia muziki wa dansi wa zamani, vijana wa kisasa nao wanaufagilia muziki wa zamani, bendi zetu zinaendelea kuishi kwa muziki wa zamani. Tungo mpya hazina nafasi, hazikubaliki.

Hii maanake yake ni kwamba wanamziki wa sasa wa dansi inawalazimu wavae makoti ya marehemu, waishi kwa kutegemea nyimbo za wasanii waliofariki, waliostaafu au wanaoelekea kustaafu. Vyombo vyetu vya habari viendelee kutawaliwa na muziki wa zamani, halafu tutegemee vipi kuchuana na muziki wa bongofleva? Tutegemee vipi kuepuka show za kiingilio kinywaji?

Bendi zinahofia kurekodi nyimbo mpya kwa sababu hazipewi nafasi kubwa kama za zamani, wasanii wapya wa dansi  wanapatikana kwa uchache sana maana hakuna nafasi kwenye bendi na hata zikiwepo hawatathaminiwa sana kutokana na imani ileile kuwa wakongwe hawana mpinzani wala mbadala.

Hii ndio tofauti kubwa ya bongofleva na dansi. Bongofleva inatoa muziki mpya kila kukicha, wasanii wapya kila kukicha, maproducer wapya kila kukicha, ubunifu mpya kila kukicha, huku hali hiyo ikiwa ni kinyume chake kwenye muziki wa dansi.Niliwahi kusema kuwa napenda sana namna wasanii wa kizazi kipya wanavyopokezana vijiti kuanzia enzi za kina Kwanza Unit, Hard Blasters, GWM, Mr II (Sugu), Sos B, Afande Sele, Mr Nice hadi kizazi cha sasa hivi cha kina Diamond, napenda namna kunavyokuwa na ving’ang’anizi wachache ambao wanatesa sokoni kwa miaka mingi, lakini napenda pia namna pumba zinavyojichuja …wanaibuka wasanii kumi, saba kati yao wanapotea, watatu wanakamata soko.

Naam. Huwezi kuzalisha shabiki mpya wa dansi kwa kumpigia nyimbo za zamani  mtoto wa kidato cha kwanza, atakuwa anaona nyota nyota tu. Katika nyimbo kumi anaweza akailewa moja tu.

Kuna kundi kubwa la watu waliouzunguuka muziki wa dansi ambao wana kasumba mbaya zaidi – eti muziki wa ukweli  ni wa zamani. Kundi hili halichangii kabisa katika kuhamasisha mabadiliko ya muziki wa dansi ili kuendana na soko la sasa.

Tunataka kuufanya muziki wa dansi uishi kwenye sayari ya peke yake, vipindi vingi vya dansi katika vituo vingi vya radio vinapiga muziki wa zamani na kufanya vipindi hivyo viwe vinazalisha aina moja tu ya wasikilizaji – Wahenga. Hakuna kitakachomvutia msikilizaji chipukizi katika vipindi hivyo.

Na kwa kuwa wasanii wa dansi wanaona nyimbo zao chache mpya wanazozizalisha hazipigwi radioni basi sasa zinaogopa hata kutuoa video mpya na kufanya vituo vyote vya televisheni vipambwe zaidi na nyimbo za bongofleva na hapo ndipo ninapozidi kujiuliza: Muziki wa dansi umebakia kuwa historia? Umebakia kuwa zilipendwa? Nyimbo nzuri za dansi zilipendwa, bendi nzuri za dansi zilipendwa, wasanii wazuri wa dansi zilipendwa, watangazaji wazuri wa dansi zilipendwa, mashabiki wa dansi zilipendwa!!!!

No comments