AYA 15 ZA SAID MDOE: ‘SORRY’ TUMEJITAHIDI SANA LAKINI MGONJWA WAKO AMEFARIKI


Daktari anapokuja kukukabali kwa uso uliojaa simanzi halafu anakuambia “samahani sana, tumejitahidi kadri ya uwezo wetu, lakini mgonjwa wako amefariki”, bila shaka kitu cha kwanza utakachotamani ni kuomba taarifa ile iwe ni njozi. Kufiwa kusikie hivyo hivyo.

Nawaza tu kuwa ipo siku moja atatokea mtu mwenye nguvu sana, au taasisi yenye nguvu halafu ituambie kuwa “tumejitahidi sana kuupigania muziki wa dansi lakini kwa bahati mbaya muziki huu sasa umekufa rasmi.”

Majuzi nilitembelewa na dansa wa TOT, Bokilo ambaye pia alipata kutesa ndani ya Twanga Pepeta, tukapata wasaa wa kujadili mawili matatu kuhusu muziki wa dansi.

Bokilo akaniambia muziki wa dansi au muziki wa rhumba kwa ujumla wake kote barani Afrika unadorora kwa sababu watunzi wa kweli wametoweka, hakuna tena tungo za maana bali kuna tungo za kujazia albam, tungo sindikizaji.

Dansa huyo akaenda mbali zaidi na kusema hata hao waliokuwa watunzi stadi ambao bado wanaendelea kufanya kazi ya muziki, uwezo wao umefika mwisho na ndio maana bendi nyingi bado zinasafiria nyota ya nyimbo zao zamani.


Niliwahi kusema kuwa kwangu mimi naamini muziki wa dansi haujafa bali unazidi kukua kwa kasi ya ajabu kiasi cha kujipenyeza kwenye aina nyingine ya muziki kama vile bongofleva, taarab na injili.

Ukifuatilia kwa makini aina hizo nyingine za muziki utagundua kuwa kwa zaidi ya asilimia 40 wanautegemea sana muziki wa dansi.

Na ni hapo ndipo ninapojiuliza, je bendi zetu zinajua kuwa zinahitaji kuzalisha mashabiki wapya kwa maana ya kizazi kipya? Mashabiki wanazeeka kiasi kwamba inafika wakati watu wanashindwa kwenda kwenye kumbi za starehe, nani anaziba nafasi zao?

Watangazaji na waandishi waliokuwa wakiunadi muziki wa dansi miaka 20 iliyopita leo hii hawapo tena – wengine wamestaafu, wengine wamefariki, wengine wamebadilishiwa majukumu na sasa zimekuja damu mpya. Je bendi zetu zimefanya juhudi za kuishawishi jamii mpya ya wana habari?

Wanamuziki nao wanapotea mmojammoja huku wakikosa warithi – kila msanii mpya wa muziki anakimbilia kwenye bongofleva na mbaya zaidi kila mmoja anataka kuwa mwimbaji. Hakuna anayetaka kujifunza kupiga chombo chochote na haitashangaza miaka 20 ijayo Tanzania ikawa haina mpiga gitaa wala ngoma.

Bendi zimekosa ubunifu wa kwenda na wakati, ziko bendi zinapiga aina ileile ya muziki kwa zaidi ya miaka 10, 15 au 20 bila kujali kuwa soko la muziki linabadilika kila wakati na kwamba walilazimika kulifuata.

Inauma sana unaposikiliza vipindi vya muziki wa kiafrika kama Weekend Bonanza, Afrika Kabisa, Afro Power, Buzuki, Tanzania Stars, Afro Rhythm na vingine vingi, vinapopiga nyimbo za wasanii wa bongofleva badala ya muziki wa bendi kama ilivyotarajiwa na wengi.

Lakini utawalaumu vipi watangazaji na waandaji wakati bendi zetu hazitaki kubadilika, hazitaki kurekodi nyimbo mpya na hata zikirekodi hizo mpya basi nyingi zinakuwa ni nyimbo uchwara. Wamiliki wa bendi hawataki kujiuliza ni kwanini nyimbo binafsi za wasanii wao zinapata muda wa kutosha redioni huku za bendi zinadorora.

Kama msanii wa bendi anaweza kutoa wimbo wake binafsi unaokidhi mahitaji ya soko na ukapigwa redioni, ni kwanini asifanye hivyo kwenye bendi yake? Ni wazi kuwa fikra zao hazikubaliki ndani ya bendi na hivyo wanaamua kutoka kivyaovyao.

Kumbi zinazidi kukauka mashabiki, watu wanakimbilia ‘club’ kucheza disco au muziki wa kizazi kipya, inafika wakati hata bendi zinazopiga bure kwenye bar hazipati mashabiki - hiyo ni dalili tosha kuwa muziki wa bendi za dansi unakufa na kama juhudi za kuzalisha mashabiki wapya hazitafanyika, basi mauti kwa bendi zetu yatakuwa hayakwepeki na tutaambiwa “sorry, tumejitahidi sana lakini mgonjwa wako amefariki!”

No comments