AZAM FC WACHEKELEA UFUNDISHAJI WA KOCHA ARISTICA CIOBA... wadai utarudisha heshima klabuni

UONGOZI wa Azam FC umefurahia mfumo unaotumiwa na kocha Mromania Aristica Cioba na kudai kuwa, utarudisha heshima ya timu hiyo msimu ujao wa Tanzania bara licha ya kuondokewa na nyota wake mbalimbali.

Kocha huyo amekuwa akitumia mfumo wa kuhakikisha wachezaji wote waliopo katika kikosi hicho wanapata nafasi ya kushuka dimbani kuonyesha viwango vyao.

Baadhi ya nyota walioiwezesha timu hiyo kupata mafanikio makubwa misimu iliyopita, ambao kwa sasa wamesajiliwa na timu nyingine ni pamoja na John Bocco, Shomari Kapombe, Aishi Manura na Erasto Nyoni, ambao ambao wote wametua Simba huku Hamis Mcha na Ame Ali wakiachwa baada ya mikataba yao kumalizika.

Akizungumza jana Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd alisema uongozi umeridhishwa kuwa kikosi walichonacho sasa kipo tayari kwa mapambano msimu ujao.

Alisema kitendo cha kikosi hicho kupata nafasi ya kujipima na timu mbalimbali kimeweza kuboresha na kuongeza matumaini mapya kwa uongozi.

“Uongozi unaamini msimu ujao utakuwa wa mavuno kwa Azam FC kwani mfumo ambao kocha amekuwa akiutumia wa kuhakikisha kila mchezaji anaingia uwanjani kuonyesha kiwango  chake umekuwa kivutio kikubwa na kambi tulizoweka nchi mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Ligi Kuu zimeweza kuwaimarisha zaidi wachezaji,” alisema Idd.

Idd alisema timu hiyo imefanikiwa kucheza michezo mingi ya kirafiki hivyo upande wa kocha ameweza kuandaa vyema kikosi chake cha kwanza ambacho atakitumia.

Idd alisema timu hiyo imefanikiwa kucheza michezo mingi ya kirafiki upande wa kocha ameweza kuandaa vyema kikosi chake cha kwanza ambacho atakitumia.


Azam FC ilianza safari ya kurejea nchini jana ikitokea Uganda ilikokuwa imeweka kambi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi huku ikiwa tayari iliweka kambi ya awali nchini Rwanda mwezi uliopita.

No comments