AZAM FC WASEMA HAWANA PAPARA NA KAGERA SUGAR KUHUSU SAKATA LA MBARAKA YUSUPH


UONGOZI wa Azam FC umewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu usajili wa mshambuliaji Mbaraka Yussuf aliyewekewa pingamizi na timu yake ya zamani ya Kagera Sugar.

Azam FC imefanikiwa kumsajili mchezaji huyo bora chipukizi wa VPL msimu uliopita kwenye usajili huu kwa mkataba wa miaka miwili na tayari ameungana na kikosi hicho kilichomaliza kambi yake ya siku 10 nchini Uganda hivi karibuni kujiandaa na msimu ujao.

Kagera Sugar inadai bado ina mkataba na mchezaji huyo kwa miaka mitatu, ikipeleka pingamizi hilo la usajili kwenye kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji ya TFF ambayo inatarajia kukutana kesho Jumapili hii kupitisha usajili.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, imeeleza kuwa timu hiyo ilimsajili mchezaji huyo kwa kufuata taratibu zote za usajili huku akidokeza kuwa tayari Shirikisho la soka la kimataifa (FIFA) limeidhinisha usajili wake kupitia mfumo mpya wa usajili wa kimtandao "TMS".

"Kagera Sugar ni timu ya muda mrefu kwenye Ligi, toka ipande haijawahi kushuka, wao wanalalamika kuwa Azam FC imemsajili mchezaji wao ambaye ni Yussuf, wakidai bado hana mkataba wa miaka mitatu."

“Lakini sisi kama Azam FC, baada ya kuamua kumsajili mchezaji huyo ni kwamba tumefuata taratibu zote na tumeona kuwa mkataba wake umekwisha na yuko huru na mkataba wa mwaka mmoja wa mchezaji huyo aliyeingia na Kagera Sugar umekwisha Juni 19 kwahiyo tayari alikuwa mchezaji huru,” alisema.

Idd alisema kuwa kwa Azam FC kuamua kumsajili Yusuph walipitia vigezo vyote na kuamini kabisa alikuwa ni mchezaji anayeweza kuichezea Azam  FC msimu ujao.

"Kingine kabisda Azam FC waliamua kupeleka jina la Yussuf kwenye usajili huu kwa maana kwenye TMS na jina lake limerudi vizuri limekubalika na FIFA baada ya kufanya usajili kupitia TMS, wenzetu wa Kagera Sugar jina la Yussuf hawakupeleka."

“Hiyo inaonyesha kuwa tayari Kagera Sugar imeshakubali mchezaji huyo mkataba wanaosema kuwa wa miaka mitatu sio wakweli na wakweli ni mwaka mmoja ulioisha, ni kweli kabisa Kagera Sugar ni wenzetu na kwenye mpira ni marafiki zetu kama kweli wamekuwa na mkataba wa miaka mitatu basi lazima na wao wangepeleka jina kwahiyo majina mawili yangepelekwa kwenye TMS."

“Na kwenye TMS yakienda majina mawili basi ni kwamba inakataa usajili na inarudisha kwa TFF kutaka ukweli kutambua kuwa mchezaji huyu sasa hivi yuko wapi, Azam FC tuna matumaini mchezaji huyu tutampata ila hatuna ugomvi na Kagera Sugar wala visasi ila taratibu za mpira zifuatwe,” alisema.

Alimalizia kwa kusema kuwa, Azam ni mojawapo ya timu zilizoandikiwa barua kufika kwenye kamati hiyo inayoshungulika na mambo ya usajili na kudai kuwa watakwenda Jumapili na vielezo vyote vinavyostahiki na wakiwa na imani kuwa suala hilo litakwisha.


Yussuf kwa sasa anaendelea na mazoezi mepesi tayari kabisa kurejea dimbani baada ya kufanyiwa upasuaji wa ngiri mwezi ulipita.

No comments