BEKI ARTHUR MASUAKU WA WESTHAM AITWA KIKOSINI TIMU YA TAIFA KONGO DRC

BEKI wa kushoto wa timu ya Westham United, Arthur Masuaku ameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Tunisia zitakazopigwa mwezi ujao.

Katika kikosi hicho kilichotangazwa juzi na kocha wa timu hiyo, Frolent Ibenge, kinahusisha wachezaji 36 ambapo baadae atachagua wanaomfaa kwa ajili ya mitanange hiyo iliyopangwa kupigwa Septemba mosi, katika uwanja wa Stade Olimpique ulioko jijini Rades nchini Tunisia na ule utakaopigwa siku tano baadae katika uwanja wa Stade de Martyrs uliopo katika mji wa Kinshasa.

Hadi sasa miamba hiyo miwili ndio inayokabana koo katika nafasi ya kwanza ya Kundi A, ikiwa imeshinda mechi zote mbili na hivyo kuwa njiani kushiriki fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Russia.


Masuaku ambaye alizaliwa mjini Lille nchini Ufaransa, amewahi kuichezea timu ya vijana ya nchini humo kabla ya kupewa kibali cha kuichezea DRC, mmoja kati ya wachezaji wapya watano ambao ni Kevin Mbabu ambaye amerejea nchini Uswisi akitokea Newcastle, kiungo mzaliwa wa Ufaransa, Tanguy Ndombele ambaye iliyopita alicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Ligue 1 akiwa na timu iliyopanda daraja, Amiens dhidi ya PSG pamoja Vital Nsimba, anayechezea timu Bourg-en Bresse inayoshiriki Ligue 2.

No comments